25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Majaliwa: Tutatekeleza ahadi zilizotolewa na JPM

MWANDISHI WETU-KILIMANJARO

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewahakikishia wananchi kwamba, ahadi zote zilizotolewa na Rais Dk. John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini zitakuwa zimetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 ifikapo mwaka 2020.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwahudumia wananchi na kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii kama maji, afya, nishati, elimu na miundombinu zinapatikana kwa uhakika.

Alitoa kauli hiyo jana, alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kituo cha Polisi  cha Tarakea wilayani Rombo, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu alisema wananchi waendelee kuwa na Serikali yao ambayo imejipanga kutekeleza ahadi zote zilizotolewa na Rais Dk. John Magufuli kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza.

Pia Waziri Mkuu alisema mtumishi mzembe, mwizi, mla rushwa na asiyewajibika hana nafasi katika Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wote waimarishe utendaji wao.

Waziri Mkuu alisema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini, hususan ya vijijini.

“Iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo, changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia, kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dk. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo itahakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji karibu na makazi yao.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kwa kushirikiana na madiwani wahakikishe wanaboresha masoko katika mipaka ya Holili na Tarakea, ili yawe katika viwango vya kimataifa.

Waziri Mkuu alisema iwapo masoko hayo yaliyo katika mpaka wa Tanzania na Kenya yataboreshwa, yatawavutia na wananchi wa Kenya kuja kufanya biashara, hivyo kuiwezesha halmashauri hiyo kuongeza mapato.

Awali, Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe, Mary, alizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Shauritanga na kisha waliweka mashada ya maua kwenye kaburi la pamoja la wanafunzi wa shule hiyo waliofariki dunia kwa ajali ya moto Juni 18, 1994.

Pia alitembelea Kituo cha Afya cha Karume kilichopo Usseri na kuzindua maboresho ya kituo hicho, ambacho kwa sasa kina uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, mama na mtoto na maabara. Baada ya hapo alitembelea Kituo cha Forodha cha Tarakea.

Kwa upande wao, wananchi waliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaboreshea huduma mbalimbali za jamii, kama upatikanaji wa dawa na vipimo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo hapo awali hazikuwa na uhakika.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles