WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema halmashauri itakayokusanya mapato chini ya asilimia 80 itafutwa.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika mkutano wa siku tatu wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT).
“Halmashauri itakayoshindwa kukusanya mapato chini ya asilimia 80 Serikali itaifuta kwa sababu jukumu la halmashauri ni kusimamia na kukusanya mapato.
“Kisheria halmashauri ni vyombo vikuu vya utekelezaji kwa kipindi cha miaka 17, hata hivyo bado halmashauri hizi hazijaweza kukusanya na kusimamia mapato yake hivyo mna wajibu wa kusimamia,” alisema Majaliwa.
Pia alisema kuna baadhi ya watumishi katika halmashauri wanamiliki kampuni za ukusanyaji wa fedha na kusababisha kuzuia matumizi ya mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki.
Alisema jambo hilo likibainika na taarifa zikathibitishwa hawatasita kumchukulia hatua za kinidhamu yule atakayekwamisha mfumo huo.
Alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatumia mfumo wa kukusanya mapato kwa njia ya elektroniki.
“Mfumo wa kielektroniki haukamiliki sababu ikiwa ni wao kulinda kampuni zao. Ikibainika hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wahusika,” alisema Majaliwa.
Katika hatua nyingine, aliwataka wenyeviti na mameya wa halmashauri na majiji kuhakikisha wanatatua migogoro ya ardhi iliyopo katika maeneo yao.
Alisema ili kuondoa migogoro hiyo, kila halmashauri ni lazima iwe na mipango bora ya kusimamia suala la ardhi.
Alisema sababu kubwa ya migogoro inayoendelea kati ya wakulima na wafugaji ni ubovu wa mifumo iliyopo katika baadhi ya halmashauri.
“Tunayo changamoto ya migogoro ya ardhi, wananchi wana malalamiko makubwa kuhusu dhuluma katika sekta ya ardhi,” alisema Majaliwa.
Aliwataka kusimamia migogoro ya hifadhi kwa kuhakikisha wanaifanya ajenda katika mikutano yao ili waweze kuitatua.
“Nendeni mkafanye mapitio, hili nimeliona Bariadi, Msata na nimelikuta Meatu na maeneo yenye misitu mikubwa, hili chukueni kama ajenda hasa katika migogoro ya hifadhi,” alisema Majaliwa.
Alisema kwa sasa bado kuna wizi na uzembe katika mamlaka za Serikali za Mitaa na hivyo kusababishwa upotevu mkubwa wa fedha.
“Sote tunakumbuka msemo wa rushwa ni adui wa haki na kwamba sitapokea wala kutoa rushwa, wananchi wanakosa haki zao za maisha kuwa duni kutokana na hali ya dhuluma, ufisadi na ujeuri wanaofanyiwa na watoaji na wapokeaji wa rushwa,” alisema Majaliwa.