Na Mwandishi Wetu-Zanzibar
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania washirikiane katika kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar na kamwe wasiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kuwagawa.
Aliyasema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika mikutano iliyofanyika Wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Kusini Unguja.
“Watanzania tusikubali mtu yeyote kutugawa kwa sababu sisi undugu wetu ni wa damu, ni vema tukaendelea kuudumisha muungano wetu, tusiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kutugawa kwani watu hao hawana tija,” alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu ambaye awali alikagua miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa maabara ya sayansi katika Shule ya Sekondari Bwejuu, mradi wa kilimo cha kisasa Jozani na kuzindua jengo la mama na mtoto Bambi alisema hayo ni matunda ya muungano, hivyo hawana budi kuendelea kuudumisha.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa maabara ya sayansi katika Shule ya Sekondari ya Bwejuu, Waziri Mkuu alitoa muda wa miezi mitatu kwa mkandarasi anayejenga maabara hiyo awe amekamilisha kazi hiyo.
Pia alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, ahakikishe watumishi wanatenga muda wa siku nne kwa wiki kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao, hususan ya vijijini.
Vilevile, aliagiza maofisa kilimo wahamishiwe vijijini ili waweze kuwasimamia wakulima, ikiwa ni pamoja na kuwashauri namna bora ya kulima kwa kufuata kanuni na matumizi mazuri ya pembejeo.
Kadhalika, alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa wananchi wote bila ya kujali dini, kabila, rangi wala itikadi za chama kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wananufaika na kuhudumiwa bila ya kubaguliwa kwa namna yoyote.
Awali, viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wakiwamo wa CUF, NRA, UPDP, NCCR-Mageuzi waliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuimarisha huduma za kijamii.
Viongozi hao walisema wapo tayari kushirikiana na Rais Dk. John Magufuli pamoja na Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa sababu viongozi hao wanafanya kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi.
“Maendeleo hayana chama, naunga mkono jitihada zinazofanywa na SMT na SMZ na nimefurahia ziara ya Waziri Mkuu hapa kisiwani Unguja na ninamuunga mkono Rais Dk. Magufuli, tumepata maendeleo ambayo hatukuyatarajia,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa NRA, Khamis Faki katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shehia ya Bambi.