MAJALIWA MGENI RASMI MKUTANO WA 14 TPSF

0
878

Na ASHA BANI, DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano wa 14 wa mwaka (AGM) wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), utakaofanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Godfrey Simbeye, maandalizi ya mkutano huo muhimu katika ustawi wa sekta binafsi nchini yamekamilika na utatanguliwa na mkutano mwingine wa wajumbe kutoka kongani 14 zinazounda sekta binafsi leo.

“Mkutano huo wa kesho (leo Jumatatu), ni muhimu sana kwani ndio utakaotoa nafasi kufanya uchaguzi wa wajumbe 14 wa bodi ya wakurugenzi ya TPSF,” alisema Simbeye na kuongeza kuwa wajumbe hao ndio watakaopendekeza majina mawili ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti wa taasisi hiyo.

Wajumbe 14 kutoka kila kongani watakaochaguliwa na kuidhinishwa kwa kawaida huwa pia ni wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), wakiungana na wengine 14 kutoka sekta ya umma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenyekiti wa Baraza.

Alisema maudhui ya mkutano wa mwaka huu ni ‘Responsible Business Leadership  for Enhanced Public Private Cooperation for Sustainable Economic Development’, yaani uongozi biashara unaowajibika katika ushirikiano wa sekta za umma na binafsi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Simbeye alisema wajumbe watakaochaguliwa kwenye mkutano wa leo watatangazwa na kuridhiwa na mkutano wa mwaka hapo kesho ambapo majina mawili yatakayopendekezwa yatachaguliwa kwenye nafasi za mwenyekiti na makamu mwenyekiti.

Katika bodi inayomaliza muda wake, Mwenyekiti alikuwa Dk. Reginald Mengi na Makamu Mwenyekiti wake, Salumu Shamte, ambao wamefanya kazi nzuri ya kuiimarisha sekta binafsi nchini.

“Ni mategemeo yetu kuwa bodi mpya itakayochaguliwa itaendeleza pale bodi inayomaliza muda wake imefanya. Serikali ina imani kubwa na sekta binafsi kama mbia muhimu wa maendeleo,” alisema Simbeye.

Alisema mikutano na vikao mbalimbali ambavyo vimefanywa kati ya sekta za umma na binafsi chini ya bodi inayomaliza muda wake, vimekuwa na mafanikio makubwa na matokeo yake yanaonekana.

“Nina furaha pia kuwajulisha Watanzania kuwa Novemba mwaka huu TPSF itaadhimisha miaka 20 tangu ianzishwe,” alisema na kuongeza kuwa yapo mafanikio ambayo yamepatikana tangu taasisi hiyo ianzishwe.

Alisema TPSF ipo mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ya kupiga vita kwa nguvu zote  vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo vimeigharimu nchi kwa kiasi kikubwa.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here