Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda madawati 1,393 ya ulinzi na usalama wa mtoto katika shule za msingi na sekondari ili kupinga ukatili dhidi ya watoto shuleni na nje ya shule.
Mheshimiwa Majaliwa amesema madawati hayo yameundwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye mikoa ya Rukwa, Arusha, Tanga, Dar es Saalam, Pwani, Shinyanga, Dodoma na Geita.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema mabaraza 560 ya watoto yameundwa kwa lengo la kutoa fursa kwa watoto kutoa maoni yao kwa uhuru na kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujieleza na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wao.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 5, 2023) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi wote wa Serikali, dini, kimila na vyama vya siasa kukemea kwa nguvu zote ushiriki wa jamii katika matendo yasioendana na mila, tamaduni na desturi za Watanzania.
“Hii ni pamoja na wazazi na walezi wote kushirikiana na Serikali katika makuzi na malezi bora ya watoto yatakayowaepusha na vitendo viovu. Serikali imeendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika ulinzi na usalama wa mtoto ili kutokomeza ukatili dhidi yao,” amesema Majaliwa.
Amesema kupitia utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (2021/2022-2024/2025), wananchi wameendelea kuhamasishwa kujitolea kwa hiari kupambana na vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kutambua wajibu wao juu ya ulinzi wa mtoto kuanzia ngazi ya familia.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Mamlaka zinazohusika chini ya uratibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kuimarisha mfumo wa ushughulikiaji wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto.