26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Ma-DED fuatilieni utendaji wa watumishi

AMON MTEGA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuweka mfumo madhubuti wa kufuatilia utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa lengo la kubaini kama wanawahudumia ipasavyo wananchi.

Majaliwa alitoa agizo hilo juzi katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Lugagala wilayani Songea.

 “Serikali inahitaji kuona watumishi wa umma wanakwenda kwa wananchi kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.

“Rais wetu Dk. John Magufuli, ni muumini wa maadili na mchapakazi ndio maana amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao, kwa sababu baadhi yao hawana uwezo wa kufikia maeneo ya kutolea huduma,” alisema Majaliwa.

Aliongeza kwa kusema kwamba ni vema kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanapanga muda wa siku tatu kwa wiki kutoka maofisini kwenda kuwahudumia wananchi hususan waishio maeneo ya pembezoni.

Katika muktadha huo aliwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali pamoja na watendaji wake waliopo kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Alisema Serikali haina msamaha kwa  watumishi wazembe, hivyo wananchi waendelee kuwa watulivu na imani kwa sababu atahudumiwa, kwamba hata ahadi zote alizozitoa Rais Dk. Magufuli zinatekelezwa.

Wakati huo huo Majaliwa alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema, asimamie zoezi la kuwaondoa wananchi wote wanaoishi na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji kwa sababu watasababisha vyanzo hivyo vikauke.

Alisema inashangaza kuona Serikali inatumia fedha nyingi kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji ya uhakika kwa wananchi halafu baadhi yao wanafanya mchezo wa kukwamisha jitihada hizo kwa kuviharibu vyanzo vya maji jambo ambalo alisema halikubaliki.

“Nakuagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea, shughulika na watu hao ambao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo hasa wale waliovamia vyanzo vya maji vya Mlima Lihanje ambako tayari kutokana na vyanzo vilivyopo Serikali imeshatumia fedha zaidi ya Sh bilioni 2, kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi ambapo sasa nimekagua vijiji viwili vya Muunganozomba na Lugagara tayari wananchi wanapata maji..

“Nimesikia baadhi yao wanaoharibu vyanzo vya maji kuwa wameenda mahakamani na wanadaiwa kuwa wameambiwa waendelee kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo hivyo, yaani hapo nashindwa hata kuwaelewa baadhi yao watu wa mhimili wa sheria kutaka kuwaruhusu watu hao huku wao wenyewe wakiwa mashahidi kwa kuona baadhi ya nchi  zilifanya mchezo na sasa zinapata tabu ya maji zinahangaika kupanda miti,” alisema Majaliwa.

Awali, Majaliwa aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Luyehela katika Kijiji cha Muungano Zomba, kuzindua kituo cha kuchotea maji cha Kijiji cha Lugagala na kukagua mradi wa ujenzi ya zahanati wa kijiji hicho.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.

Wengine ni Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme na maofisa wengine wa Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles