MAJALIWA: KISWAHILI NI TUNU, LULU YA TANZANIA

0
584
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia),akimkabidhi Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu nakala ya Kamusi Kuu ya Kiswahili mara baada ya kuizindua.

Na Eleuteri Mangi – MAELEZO


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia),akimkabidhi Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu nakala ya Kamusi Kuu ya Kiswahili mara baada ya kuizindua.

Kuzinduliwa kwa Kamusi Kuu ya Kiswahili hivi majuzi, bungeni mjini Dodoma, imekuwa ni chachu katika kukuza na kusimamia matumizi sahihi na fasaha ya lugha hii miongoni mwa watumiaji wake.

Uzinduzi wa kamusi hiyo ni ishara njema ya kukijenga na kukiimarisha Kiswahili ili kiweze kutumika kwa ufasaha katika nyanja zote za maisha ikiwemo  elimu katika ngazi zote, kijamii, kisiasa na kiuchumi ndani na nje ya nchi.

Akizindua kamusi hiyo mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasisitiza Watanzania  kujivunia kilicho chao kwa kuitumia lugha hii katika shughuli zote rasmi za kitaifa ikiwamo mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.

Hakika lugha ya Kiswahili imeendelea kuwa ngao na nguzo muhimu kwa ustawi wa taifa na katika kulinda umoja wa kitaifa kwa Watanzania kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Kutokana na umuhimu wake,  Waziri Mkuu anasema; “Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa kitaifa. Hakika lugha hii ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo, tuithamini kwani ni lulu na tunu ya Taifa.”

Zaidi ya hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kutumia lugha ya Kiswahili na kutoa mfano ambapo rais alitumia lugha hiyo kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika mwaka 2017.

“Rais alitumia Kiswahili kuhutubia mkutano huo na amekuwa  akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo lake ni kuitangaza lugha hii,” anasema Majaliwa.

Watanzania tuna kila sababu ya kumpongeza Rais kwa raghba, uzalendo, jitihada na uungwana kwa kujivunia kutumia lugha ya Kiswahili kama utambulisho wa Taifa na utamaduni wa Mtanzania.

Hatua hiyo ya Rais Dk. Magufuli imeshadidisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kuwa mwanzo mpya kwa viongozi na jamii kuipenda na kuitumia mara zote wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ya kitaifa na kimataifa.

Mafanikio ya kuandika na kuchapisha Kamusi Kuu ya Kiswahili si ya kubeza, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limeendelea kuwa kisima cha hazina ya lugha hii na wanapaswa kupongezwa na kutiwa moyo kwa kazi hii nzuri na kuwa  mstari wa mbele katika kusimamia.

Awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi zaidi barani Afrika, pia ni lugha ya 10 kati ya 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Aidha, katika hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2017/2018 aliyowasilisha bungeni, Dk. Mwakyembe alisema BAKITA imepewa jukumu la kulinda na kukuza lugha ya Kiswahili ambapo pamoja na mambo mengine, Kamusi ndiyo mzizi wa lugha na wamefanikiwa kuratibu na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa asasi na mashirika mbalimbali, watu binafsi pamoja na mikutano ya kimataifa.

Hatua ya ukusanyaji wa Istilahi 300 za magonjwa ya mimea kwa ajili ya Kamusi ya  magonjwa ya mimea; kuhariri kamusi ndogo za lugha tatu ambazo ni Kiswahili-Kiingereza-Kifaransa, Kiswahili-Kiingereza-Kireno na Kiswahili-Kiingereza-Kiarabu imedhihirisha umahiri wa  BAKITA katika usimamizi na ulezi wa lugha hii.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, katika hotuba yake iliyosomwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo Azzan Zungu wakati wa uzinduzi wa Kamusi hiyo alisema, Bunge linaendelea kusimamia matumizi ya Kiswahili katika shughuli zake za kila siku na kusisitiza kuwa Bunge litakuwa kituo cha maendeleo ya Kiswahili.

Akitoa taarifa kabla ya kuzinduliwa kwa kamusi hiyo, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Dk. Seleman Sewangi alisema imeundwa kwa lugha ya Kiswahili na ina jumla ya maneno 45,500 ambapo kazi ya kuiandaa ilianza Agosti 12, 2011. Kamusi hiyo ilikamilika na kuchapishwa toleo la kwanza mwaka 2015.

Naye Balozi wa Kiswahili Afrika, Mama Salma Kikwete amewaasa Watanzania kutumia kamusi hiyo ili kujiongezea elimu kuhusu lugha hii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here