27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Jukumu la Usalama barabarani ni la kila mtu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa jukumu la usalama barabarani ni la kila mtu na si la Serikali pekee na amewataka wananchi wote watoe ushirikiano kuzuia ajali za barabarani.

“Jukumu la usalama barabarani ni la kila mmoja wetu na si la Serikali pekee. Hivyo basi, tushirikiane kupambana na kuzuia ajali za barabarani kwa kumuonya kila mmoja wetu anapovunja sheria na kanuni za usalama barabarani. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kupunguza ajali za barabarani na kuokoa maisha,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Machi 14, 2023 wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria uzinduzi wa Wiki ya Usalama Barabarani Kitaifa uliofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza.

Akiainisha makundi yanayochangia kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani, Waziri Mkuu amesema uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaonesha kuwa mabasi yanayofanya safari ndefu ndiyo wahusika wakubwa wa ajali za barabarani.

“Ajali hizo kwa kiwango kikubwa husababishwa na uzembe wa madereva. Ni kwa nini basi tusifuate sheria zilizowekwa kama vile kuhakikisha kuwa kwenye mabasi hayo kuna madereva wawili watakaokuwa wanapokezana? Naliagiza Jeshi la Polisi wasimamie hili na wenye mabasi wahakikishe kuwa wanaajiri madereva zaidi,” amesema Majaliwa.

Amesema kuwa madereva wa magari na pikipiki nao wamekuwa ni sehemu kubwa ya vyanzo vya ajali za barabarani na kuchangia kuongezeka kwa ajali kwa kuendesha kwa mwendo kasi, kuyapita magari ya mbele bila ya kuchukua tahadhari, kuendesha magari mabovu ama kutoheshimu alama na michoro ya barabarani.

Katika kuhakikisha ushirikiano miongoni mwa wadau unakuzwa na mapambano dhidi ya ajali za barabarani yanaimarishwa, Waziri Mkuu ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani liharakishe mchakato wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuwe na sheria bora isiyoacha mwanya kwa watumiaji wa barabara na waendesha vyombo vya moto.

Pia amelitaka Baraza hilo lifuatilie kuanzishwa kwa mfumo wa kuweka alama kwenye leseni za udereva (points system) ili kuwaondoa madereva wanaokithiri kwa kukiuka sheria na kuwafungia kuendesha vyombo vya usafiri wale watakaoonesha usugu.

Kuhusu maagizo yaliyotolewa kwenye sherehe za mwaka jana mkoani Arusha, Waziri Mkuu amesema:

“Harakisheni kutekeleza maagizo ya Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu kuimarisha ukaguzi wa magari kwa kuishirikisha sekta binafsi badala ya utaratibu mnaoendelea nao sasa,” amesema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles