Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema jitihada za pamoja zinahitajika ili kutokomeza vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vikiwemo vya ukeketaji kwani madhara yake ni makubwa.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum isimamie utekelezaji wa mipango na mikakati mahsusi ya kutokomeza ukeketaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 18, 2022) wakati akiahirisha Mkutano wa Sita wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 5, 2022.
Amesema vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto vinaendelea licha ya uwepo wa afua mbalimbali za kuelimisha wananchi kuhusu madhara yake.
Ameongeza kuwa mikoa inayoongoza kwa vitendo vya ukeketaji ni Manyara (asilimia 58), Dodoma (asilimia 47), Arusha (asilimia 41), Mara (asilimia 32) na Singida (asilimia 31).
Amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa bado suala hilo ni changamoto kwa nchi yetu, hivyo ametoa wito kwa viongozi mbalimbali kuhamasisha wananchi kupinga vitendo hivyo vya ukatili.
“Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Viongozi wa Dini na wadau wote kuunganisha nguvu na kukemea vitendo hivyo, pia hatua kali zichukuliwe kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo,” amesema Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuuameliagiza Jeshi la Polisi nchini liongeze nguvu ya kiulinzi hadi kwenye ngazi ya kata, kufanya operesheni na misako ya kuwabaini wahalifu wote.
“Fanyeni operesheni na misako ya kuwabaini wahalifu wote wakiwemo waganga wanaopiga ramli chonganishi na kuchukulia hatua askari, wakaguzi na maafisa wasio waadilifu,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kujitokeza kwa matukio mbalimbali ya hivi karibuni yanayohusisha mauaji ya raia kwa raia, moto kwenye masoko na baadhi ya raia kujinyonga.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa taasisi za dini waendelee kusaidia katika suala zima la malezi ya kiroho ili kujenga jamii yenye uchamungu na uadilifu.