Na TUNU NASSOR
DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa, amewataka waumini wa dini mbalimbali kujiepusha na kauli na vitendo vitakavyopandikiza chuki dhidi ya dini au waumini wa dhehebu jingine ili kuondoa mifarakano katika jamii.
Akizungumza wakati wa kilele cha mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana, Majaliwa alisema kupandikiza chuki na uhasama wa dini hakuna atakayeibuka mshindi.
“Niwaombe waumini wa madhehebu mbalimbali wadumishe amani kwa kuendelea kuvumiliana katika tofauti zao za imani na itikadi ili kila mmoja apate fursa ya kufanya ibada bila hofu,” alisema Majaliwa. .
Aliwataka Watanzania kuwalea watoto katika misingi ya dini wewe raia wema na wapambanaji dhidi ya dhuluma kwao na kwa nchi yao.
“Simamieni nidhamu ya watoto na kuhakikisha wanapata elimu stahiki iwe urithi wao na taifa, fuatilieni mienendo yao wasijiingize katika matumizi ya dawa za kulevya na vitendo viovu vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na ustawi wa taifa,” alisema Majaliwa.
Aliwataka waumini kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ikiwa pamoja na kuwafichua wakwepa kodi.
“Kila mmoja ahakikishe analipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria kuisaidia serikali kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema.
Majaliwa pia amemtaka meya na mkurugenzi wa manispaa ya Temeke kuangalia namna ya kuiongezea eneo Taasisi ya Al Hikma ili kupanua shughuli zake.
Naye mlezi wa Taasisi ya Al Hikma, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema jukumu lake kama mlezi wa taasisi hiyo ni kuwakaribisha wageni waliofika katika shughuli hiyo.
“Umri umeninyang’anya maneno ya kusema ninachoweza kusema ni kwamba naafiki na kuunga mkono yote yaliyozungumzwa hapa,” alisema Mwinyi.
Katika mashindano hayo, idadi ya Juzuu tatu, tano, 10, 20 30,, mtoto kutoka Somalia Mohamed Abdullahi Aden(12) aliibuka kidedea kwa kundi la Juzuu 30 na kuzawadiwa Sh milioni 15.75.
Naye Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir ameonya Waislamu kuwatumia Waislamu wenzao dhidi ya wengine kwa sababu Quran haijaelekeza kuua nafasi ya mtu mwingine.