26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Majaliwa: Imarisheni hali ya usalama

Mwandishi Wetu -Zanzibar

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,  kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa ili kuboresha shughuli za utalii na kulinda usalama wa raia na mali zao.

Pia amemwagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ahakikishe Jeshi la Polisi linadhibiti mianya yote ya uingizwaji, usafirishwaji, uzalishaji na utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na vitendo vya ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Hayo aliyasema juzi wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwenye ukumbi wa mikutano wa Hotel Verde, ambapo alisistiza watumishi kutimiza majukumu yao ipasavyo.

“Huu ni mji wa kitalii, hivyo ni lazima polisi wakaimarisha hali ya usalama, vitendo vya wizi na uporaji lazima vidhibitiwe. Pia halmashauri ya Jiji nayo ihakikishe hali ya usafi inaimarishwa hususani katika barabara. Mji huu lazima uvutie,” alisema Majaliwa

Wakati huo huo,Waziri Mkuu amesema hali ya ufaulu kwa upande wa elimu ya msingi si nzuri, ambapo ameuagiza uongozi wa wizara ya elimu uhakikishe unafanya mabadiliko katika kuisimamia sekta hiyo.

“Maofisa elimu waache kukaa maofisini waende mashuleni kusimamia ufundishaji,” alisema

Alisema Serikali inataka kuona watoto wakifanya vizuri kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi elimu ya juu. “Ili malengo hayo yatimie ni lazima watendaji katika sekta ya elimu wakabadilika na kusimamia vizuri ufundishwaji.

“Tunataka watoto wanapoanza masomo yao ya msingi wafike hadi ngazi  ya chuo kikuu ili tuwe na wataalamu wengi,” alisema

Akizungumzia kuhusu sekta ya afya, Waziri Mkuu amewataka watumishi waimarishe utoaji wa huduma hizo kwa wananchi kwa sababu Serikali imefanya mabadiliko kwenye sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya dawa.

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mjini Magharibi, ufanye tathmini ya utendaji wake na kubaini mafanikio yanayopatikana katika ukusanyaji wa mapato pamoja na changamoto zitakazojitokeza ili waweze kupatia ufumbuzi kwa wakati.

Alisema ni vema wakasimamia makadirio ya ukusanyaji wa mapato na wahakikishe wanabaini vyanzo vyote na wafuatilie iwapo makadirio hayo ni sahihi na fedha zote zinazokusanywa kama zinaingia katika mfuko mkuu wa Serikali, makusanyo yafanyike kielektroniki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Khatibu, amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba maelekezo yote aliyotoa kwao ameyapokea na kwamba watayafanyia kazi ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,625FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles