23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa azindua mpango wa Tatu wa Maendeleo

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 utakaogharimu Sh trilioni 114.8, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia Sh trilioni 40.6 na sekta ya umma Sh trilioni 74.2.

“…fedha hizo zinajumuisha mikopo na misaada ya wabia wetu wa maendeleo. Kwa niaba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, napenda kuwahakikishia kwamba fedha hizi zitapatikana na malengo tuliyojiwekea yatatekelezwa,” amesema Majaliwa.

Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 29, 2021) wakati akizindua Mpango huo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Amesema mpango huo una dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu na umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.

Amesema Serikali itahakikisha malengo ya Mpango huo yanafikiwa.

“Kamwe hatutafumbia macho tabia ya ukwepaji kodi, kazini, ufujaji wa fedha na rushwa na tutaendelea kuenzi bunifu na kupokea mawazo mbadala yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa Mpango huu,”amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za serikali za kuimarisha upangaji mipango na kusimamia rasilimali za ndani ya nchi ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, ardhi, fedha na rasilimali watu kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.

Amesema ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo yaliyopangwa, Wizara imeandaa mwongozo wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi na programu za maendeleo na mfumo wa kitaifa wa kusimamia miradi ya maendeleo.

Naye, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Christine Musisi amesema wananchi, serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi watautumia mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Pia ameihakikishia Serikali kwamba mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yataunga mkono utekelezaji wa mpango huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles