31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AWATAKA MADIWANI TABORA WAACHE KUFANYA BIASHARA NA MANISPAA

Na Mwandishi Wetu – Tabora                 |                


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wasifanye biashara na halmashauri hiyo kwa kuwa wanakiuka maadili ya utumishi wa umma.

Agizo hilo alilitoa mjini hapa jana alipozungumza na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Manispaa ya Tabora na Hospitali ya Rufaa ya Kitete.

“Madiwani mjiondoe kuwa wasimamizi wa kampuni zinazofanya kazi na halmashauri yenu, na wakuu wa idara nanyi muwe makini, mfanye kazi na kampuni huru ili mchukue hatua pale linapotokea tatizo.

“Nyie madiwani ndio mnaopaswa kuisimamia halmashauri, sasa kama watu mliopewa dhamana mkiingia kufanya shughuli nyingine, mnawakwaza wakuu wa idara na kuharibu mambo. Fanyeni kazi yenu ya kuisimamia halmashauri kwa mujibu wa dhamana mliyopewa,” alisema.

Alisema madiwani wawe wanafanya tathimini ya ushauri unaotolewa na wakuu wa idara na wasijihusishe na biashara ndani ya halmashauri zao na badala yake waziachie kampuni zifanye kazi zenyewe na Serikali bila ya kuzisimamia.

Alitolea mfano wa mradi wa ununuzi malori mawili na makontena 20 ya kukusanyia taka mitaani ya manispaa hiyo, na kampuni inayomilikiwa na diwani ilipewa zabuni ya kununua vifaa hivyo na ilipokabidhi, lori moja lilikuwa bovu na kukataliwa.

“Yeye akaenda kulipaka rangi na kuwaletea, walilikataa tena,” alisema.

Katika hatua nyingine, alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu, aifanyie uchunguzi Ofisi ya Mwekahazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Abbas Mwanzori, baada ya kuwapo kwa utafunaji wa fedha za umma kwa visingizio mbalimbali.

Alisema zaidi ya Sh milioni 12.4 zimelipwa na Mwanzori kwa malipo ya wahasibu waliofanya kazi muda wa ziada na watumishi, huku kukiwa hakuna fomu zilizojazwa na watumishi hao.

“Hatuwezi kwenda mbele tukiwa na watu wa namna hii. Halmashauri haiwezi kuendelea, mtu anatumia vibaya ofisi kwa manufaa yake binafsi. Kati ya fedha hizo, Sh milioni 8.4 mlizitoa kwa kutumia password ya Halima (Mhasibu) bila ya kumjulisha na alipogundua akahoji mkamuhamishia sokoni, naagiza arudishwe mara moja,” alisema.

Pia aliwataka watumishi wa umma wajikite katika kufanya kazi vizuri na watambue dhamana waliyopewa na Serikali, ambayo ni kuwatumikia wananchi wa Tabora na si vinginevyo.

“Tunahitaji kuona mabadiliko ya maendeleo kwenye maeneo yenu ya kazi,” alisema.

Aliwaeleza watumishi hao kuwa ili waweze kupata mafanikio ya kiutendaji, lazima wawe na mpango kazi utakaomwezesha kila mmoja wao kutimiza wajibu wake.

Pia aliwaagiza wakuu wa wilaya wasimamie utendaji wa pamoja katika idara zilizo ndani ya halmashauri zao, na wahakikishe watendaji hao wanawatembelea wananchi katika maeneo yao ili wanapokutana katika mabaraza ya madiwani wafanye tathmini ya kina juu ya mafanikio na changamoto zinazowakabili wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles