22 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Majaliwa awaaga watalii 1,000 kutoka Israel

Na Mwandishi Wetu

-Kilimanjaro 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watalii kutoka Israel wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania pindi watakaporudi nchini mwao.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati akiwaaga watalii 274 walioondoka kurejea kwao.

Watalii hao ni miongoni mwa watalii 1,000 waliowasili nchini tangu Aprili 20, mwaka huu na kutembelea maeneo kadhaa ya vivutio katika Ukanda wa Kaskazini.

Majaliwa aliwaomba watalii hao wapange muda wao na watafute fursa nyingine ya kuja Tanzania kutembelea mbuga nyingine za Ukanda wa Kusini fukwe za Zanzibar. 

 “Tumefarijika na ujio wenu na tunaamini mtaenda kutangaza mazuri mliyoyaona kwa wengine. Tunazo mbuga nyingine za Rubondo, Katavi, Ngorongoro, Ruaha, Selous, fukwe nzuri za Zanzibar na Mlima Kilimanjaro,” alisema. 

Pia aliwashukuru mawakala wa utalii nchini pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Another World kutoka Israel, Carmel Shlomo kwa kuamua kuitangaza Tanzania kama kivutio namba moja cha utalii barani Afrika. 

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, aliwashukuru watalii hao kwa kuamua kuitembelea Tanzania licha ya kuwa wangeweza kwenda maeneo mengine yaliyo jirani na Israel. 

 “Natambua uchovu mlionao sababu ya urefu wa safari kutoka Israel hadi hapa, lakini nawashukuru kwa uamuzi wenu wa kuja Tanzania katika kipindi hiki ambacho tunafanya maboresho katika sekta ya utalii ili tutoe huduma bora zaidi,” alisema. 

Alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii na hii inawezekana kwa sababu iliamua kutenga zaidi ya robo ya ardhi yake kwa ajili ya mbuga na hifadhi za taifa za wanyama.

Pia alizishukuru kampuni za utalii za Tanzania na Israel kwa kushirikiana kuleta watalii wengi kiasi hicho. 

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Excellent Guides, Mauly Tours and Safaris, Matembezi, Leopard Tours and Safaris, African Queen Adventures na Tawisa zote za Tanzania na zile kutoka Israel ni Another World, My Trip, Camel na Safari Company.

Kwa upande wao, baadhi ya watalii kutoka Israel walisema wamevutiwa na waliyoyaona hapa nchini na wameahidi kurudi tena ili watembelee vivutio vingine zaidi. 

Naomi Moscovich na mabinti zake Dana na Lihi, walisema wamevutiwa na wingi wa wanyama waliowaona, lakini pia wameguswa na ukarimu wa watu waliokutana nao. 

 “Tunaondoka na neno moja kubwa nalo ni kwamba hatutaisahau Tanzania na tutarudi tena hivi karibuni,” alisema Dana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,504FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles