30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AVUNJA BODI WETCU, VIONGOZI MBARONI

Na Mwandishi Wetu-TABORA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa,  amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa  Tabora kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU)   na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

Pia Waziri Mkuu amevunja Bodi ya WETCU   na  Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB)  kwa   kushindwa  kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Agizo hilo alilitoa jana mjini Tabora katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa bodi na Serikali.

Alisema    Rais Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa TTB, Vita Kawawa pamoja na Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Wilfred Mushi.

Viongozi wa WETCU ambao Waziri Mkuu ameagiza wakamatwe ni Mwenyekiti, Mkandara Mkandara, Makamu Mwenyekiti, Msafiri Kassim, Mkaguzi wa Ndani na Mhasibu  Mkuu.

Pia alitangaza kuwasimamisha kazi watumishi wa kitengo cha uhasibu wa chama hicho hadi uchunguzi utakapokamilika.

“Kuanzia sasa watumishi wote wa kitengo cha uhasibu pamoja na menejimenti nimewasimamisha kazi pamoja na Mrajisi wa Mkoa wa Tabora, Deogratius Rugangila. “Kamanda hakikisha ofisi hazifunguliwi kuanzia sasa hadi hapo timu ya ukaguzi  itakapokamilisha kazi yake,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alisema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na Bodi ya Tumbaku Tanzania jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.

“Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea Sh bilioni 15 ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni Sh bilioni 10 ambazo hawajazikatia risiti.

“Wakati wanachama ambao ni wakulima wakiendelea kutesema WETCU walinunua gari la Sh milioni 269 kinyume na na maelekezo ya mkutano mkuu wa wadau ambao ulipitisha zitumike Sh milioni 40 tu,” alisema.

Alisema WETCU kimekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha.

Alitoa  mfano wa ukarabati wa ofisi tatu ikiwamo ya makao makuu ambayo ilipangwa ikarabatiwe kwa Sh milioni 33 wakatumia Sh milioni 170 na ofisi za Tabora na Urambo zilipangiwa Sh milioni tano kila moja lakini  hazikukarabatiwa.

  Waziri Mkuu pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, wakuu wa wilaya zote za mkoa huo  na maofisa kilimo na ushirika kuhakikisha wanasimamia vizuri zao hili  liweze kuwa na tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles