26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa atoa maagizo mapya kwa Tanroads

Morogoro

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kuacha tabia ya kukaa ofisini na badala yake kufanya ukaguzi wa kina wa barabara na madaraja katika maeneo yao mara kwa mara.

Majaliwa aliyasema hayo baada ya kutembelea na kukagua hatua za ujenzi wa barabara ya mchepuo aliyoagiza ijengwe na Tanroads Machi 4 ili kuondoa msongamano wa magari yaliyokwama kwa siku tano  katika barabara ya Dodoma-Morogoro.

“Nimepita mara ya pili kukagua hatua za ujenzi na nimeridhika kuona maendeleo yake, barabara hii ya mchepuo imeondoa foleni iliyokuwepo,” alisema  Majaliwa.

Aliwasihi mameneja wa Tanroads kuhakikisha wanakagua vipenyo vya madaraja yote, hususani ya muda mrefu kuona kama ukubwa wake unaruhusu maji kupenya kwa urahisi, hasa vipindi hivi vya mvua nyingi. 

Aliitaka Wizara na Tanroads kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa matengenezo zinatumika kikamilifu ili kuboresha mawasiliano katika barabara kuu na kuhakikisha zinapitika majira yote ya mwaka.

Alitoa wito kwa wananchi wote kuwa wavumilivu katika maeneo yaliyopata athari za mvua, hasa katika barabara na madaraja wakati Serikali inafanya utaratibu wa ukarabati wa miundombinu.

“Tunaelewa mvua zinanyesha, hivyo nawaasa Watanzania kuwa watulivu wakati kazi ya ukarabati zinafanyika kwa dharura kwanza hadi hapo hizi mvua zitakapoisha,” alisema Majaliwa.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa kalavati la zege katika eneo la Kiyegeya, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, alisema ujenzi wa awali waliweka makalavati ya chuma yenye urefu wa mita 12 kila moja kwa dharura ambayo yaliwezesha magari kupita njia moja.

Mfugale alisema kazi inayoendelea sasa ni ya kujenga kitako na kuunganishwa na kalavati la awali ili kuwezesha magari mawili kupita kwa pamoja. 

“Hivi sasa magari yanayotoka njia ya Morogoro yanapita katika njia ya awali na yanayotoka Dodoma yanapita njia ya mchepuo ili kuruhusu ujenzi kuendelea,” alisema Mfugale.

Alisema kazi hiyo ya ujenzi inatarajia kumalizika baada ya wiki mbili ili magari yaweze kutumia njia ya awali wakati wanaendelea na ujenzi wa tabaka la lami.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles