25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ataka wananchi kujitokeza kampeni Uchaguzi Serikali za Mitaa

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kila Mtanzania atapata haki yake ya msingi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24.

Aidha, amewataka wananchi kwenda kusikiliza sera za wagombea ili wapate nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka kuwaongoza kwenye maeneo yao.

Majaliwa aliitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo yaliyoulizwa na wabunge, akiwemo Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula (CCM).

Katika swali lake, Kiula alisema kwa kuwa kumekuwa na malalamiko kwenye maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wapo watu ambao wana hofu ya kukosa haki zao za msingi za kupiga au kupigiwa kura.

Kiula alihoji ni nini kauli ya Serikali katika kuhakisha hofu hiyo inaondoka.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema katika uchaguzi huo kulikuwa na maandalizi ya kujiandikisha, kuchukua na kurudisha fomu na yameshakamilika.

Alisema kuwa kinachosubiriwa sasa ni kuanza kwa kampeni za wagombea Novemba 17 ili kila mmoja akaeleze namna atakavyoshirikiana na wananchi.

Majaliwa alisema baada ya hapo, Novemba 24 Watanzania wote watatumia haki na fursa yao kuchagua kiongozi wanayemtaka.

“Kwa utatibu huu unaoongozwa na kanuni na utaratibu, tunaamini kila mmoja atapata haki yake ya msingi.

“Muhimu ni kuzingatia kanuni na sheria na taratibu ili uweze kutimiza azma ya kumchagua kiongozi ambaye unamtaka katika eneo ulipo, kitongoji au mtaa,” alisema Majaliwa.

Alitoa wito kwa Watanzania kuwa kipindi kinachokuja cha kampeni waende kusikiliza sera za wagombea ambao wana nia thabiti ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao, hivyo kila mmoja apate nafasi ya kumchagua kiongozi anayemtaka.

Katika hatua nyingine, Majaliwa  amewataka wafanyabiashara nchini kuhakikisha wanahamisha chakula kutoka maeneo yenye chakula cha kutosha na kupeleka maeneo yasiyo na chakula ili kujipatia kipato.

Majaliwa alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) ambaye katika swali lake alihoji hali ya upatikanaji wa chakula maeneo mbalimbali nchini.

“Kiapo chetu kinatutaka tuwe wakweli, na nitasema ukweli daima. Baadhi ya mikoa ikiwamo Dodoma na wilaya zake zote, Manyara, Singida na baadhi ya mikoa inakabiliwa na uhaba wa chakula.

“Baadhi ya wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wa mikoa inawezekana hawatoi taarifa sahihi kwa sababu ya woga, kutokana na kuwa pengine kuelewa vibaya kauli ya Rais.

“Je, Serikali iko tayari sasa pengine kuunda tume au kamati maalumu ifanye utafiti ije na taarifa sahihi ya upungufu wa chakula katika maeneo haya, ili wananchi hawa wapelekewe chakula kwa bei nafuu, kwa sababu hali siyo shwari?” alihoji Nkamia.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema; “Tanzania ina maeneo tofauti na kuna maeneo yanapata mvua nyingi na yamezalisha chakula cha kutosha, yapo maeneo hakuna mvua na hakuna chakula cha kutosha.”

Alisema kuwa ni jukumu la wafanyabiashara kufanya biashara, kuhamisha chakula kutoka maeneo yenye chakula cha kutosha na kupeleka maeneo ambayo hayana chakula ili kujipatia kipato.

“Wakuu wa wilaya na mikoa pindi wanapokutana na hali hii, wakutane na wafanyabiashara wawashawishi kuchukua chakula kutoka maeneo yenye chakula na kuwaletea,” alisema Majaliwa.

Alisema kuwa upungufu wa chakula upo katika baadhi ya wilaya na maeneo kadhaa kulikotokana na tatizo la hali ya hewa.

“Kuna baadhi ya maeneo hatukupata mvua za kutosha, jambo hili linapotokea kwenye maeneo husika, tuna viongozi na tumeweka utaratibu kama Serikali kwa viongozi walioko katika maeneo hayo kuweka utaratibu,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali ina chombo kinachonunua chakula na kuhifadhi NFRA, baada ya kununua hupeleka katika maeneo ambayo yana upungufu wa chakula na kuyauzia.

“Hofu aliyonayo mbunge huyo ni kwamba ni pale Rais alipoagiza kuna hali nzuri ya hali ya hewa kila mmoja ana nafasi ya kwenda kulima, alafu kunakuwa hakuna chakula. Sasa hapo yale maelekezo yanachukua nafasi yake.

“Inapotokea kuna hali ya hewa mbaya, mkuu wa wilaya ataeleweka tu, timu itaenda kuona hali halisi na kuweza kuzungumza nao ili waweze kupata chakula kwa bei nafuu,” alisisitiza.

Vilevile, Majaliwa amewaahidi wananchi kuwa mkakati wa kujenga miundombinu utakwenda sambamba na kuajiri wataalamu wapya katika sekta ya elimu.

Majaliwa alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid  Shangazi (CCM), ambaye alisema sekta ya elimu na afya zina upungufu mkubwa sana wa watumishi.

Alihoji nini mkakati wa Serikali kuhakikisha tunapata watumishi wa kutosha kwenda kuwahudumia Watanzania, ili dhana ya kupeleka huduma kwa Watanzania inatimia?

Akijibu swali hilo, Majaliwa alikiri kuwa ni kweli sekta hizo mbili zina mahitaji mengi ya watumishi kwa sababu huduma zimepelekwa hadi ngazi ya vitongoji.

Alifafanua kuwa ukweli mwingine ni kuwa wamefanya maboresho ambapo sera inaeleza kuwa kila kata kuwe na zahanati, kila wilaya kuwe na hospitali.

Majaliwa alisema kitu ambacho Serikali inafanya ni kuongeza watumishi kwa sababu kadiri wanavyoongeza miundombinu ni lazima suala hilo lizingatiwe.

“Serikali imeanza kutoa vibali vya ajira katika sekta hizi mbili za afya na elimu, hata kwenye kilimo.

“Mwaka jana tuliajiri watumishi 6,000 na sasa tuna kibali ambacho kitatoka hivi karibuni cha watumishi 16,000 kwa upande wa sekondari na msingi,” alisema.

Alisisitiza kuwa wanaamini baada ya ajira hiyo kwenye shule za sekondari na elimu watakuwa wamepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa walimu, hivyo hivyo kwenye sekta ya afya wanataka kuhakikisha wanapeleka wataalamu wa kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles