27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ataka vijana kushirikishwa shughuli za maendeleo

Mwandishi wetu -Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewaagiza watendaji wa ngazi zote wahakikishe vijana wanawezeshwa kushiriki shughuli za maendeleo.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa, viwanja vya Mpilipili, nje kidogo ya mji wa Lindi.

 “Vijana tushirikiane na Serikali na kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za Serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na John Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo.

“Hatua hii itatuwezesha kama taifa tuvuke na tufikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Majaliwa.

Alisema  wakati anatembelea mabanda ya maonyesho, ameona ubunifu wa kijana ambaye ameunda mashine ya kumsaidia mtoto njiti apate joto na pia amemuona kijana mwingine ambaye amebuni mtambo wa kupukuchua magunia 100 ya mahindi kwa saa moja.

 Pia alitembelea banda la kikundi cha vijana kutoka China, Korea Kusini, Argentina, Azerbaijan na Tanzania ambao waliishi kwenye mazingira magumu na wakabadilika na wameamua kushiriki maonyesho hayo ili kuwabadilisha mtazamo vijana wenzao.

 “Nimefurahi kuwaona hawa vijana, ninaamini watashirikiana na wenzao wa hapa kuwabadilisha vijana wa Tanzania ili wawe na fikra endelevu,” alisema.

Akizungumzia mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi, Majaliwa alisema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini, imeanza kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhouse) katika mikoa yote na halmashauri zote nchini.

 Alisema teknolojia hiyo itawasadia wakulima kupata mazao mengi katika eneo dogo na kupata mazao bora yanayokidhi viwango katika soko la ndani na nje ya nchi.

“Kwa kutumia teknolojia hii, vijana wengi watapata ajira katika sekta ya kilimo,” alisema Majaliwa.

 Wakati huohuo, Majaliwa alisema Serikali imeziagiza halmashauri zote nchini zitenge maeneo maalumu kwa shughuli za vijana, ikiwa ni pamoja na maeneo ya ujenzi wa viwanda vinavyomilikiwa na vijana.

 “Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, hadi mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya ekari 217,882.36 zilikwishatengwa. Ninaziomba halmashauri zote zisimamie na kutekeleza agizo hilo ili kuhakikisha maeneo hayo yanatumiwa kama ilivyokusudiwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles