26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ATAKA UADILIFU KUANZIA NGAZI YA FAMILIA

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wazazi wana jukumu la kulea watoto katika misingi ya kumcha Mungu taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi.

Kauli hiyo aliitoa juzi alipozungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Alisema wazazi wanapaswa kujitathmini juu ya malezi ya watoto wao na kujihoji kama wamepata malezi yanayostahili.

“Kupitia mafunzo tuliyoyapata leo, tujitathmini kuhusu makuzi ya watoto wetu. Je, watoto wetu wanapata malezi stahiki? Je, tunawalea katika misingi ya kutoa kwa ajili ya Mungu au tunawafundisha wajilimbikizie mali?

“Je, tunawahoji watoto wetu kuhusu utajiri wanaoupata ghafla  au tunawapongeza na kufurahia bila kujua wanapata wapi utajiri huo?” alihoji na kuongeza:

“Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu   kuwa na taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe  tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema Majaliwa.

Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo  Pinda.

Mzee Xavery Pinda alifariki dunia Novemba 27 mwaka jana katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kuzikwa kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele, Katavi.

“Nitumie nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya taifa tunalotaka kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisema.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia Sh milioni 10 ambako   Sh milioni 160 zilikusanywa.

Awali,  akiongoza ibada ya shukrani, Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padri Chesco Msaga alisema kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu kwa sababu  hakuna mwanadamu anayeweza kudai kuwa yuko jinsi alivyo kwa sababu ya akili zake.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda alisema harambee hiyo inafuatia uamuzi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya wa kuiteua Zuzu iwe parokia.

“Kikubwa tunachopaswa kufanya kufuatia uamuzi huo ni kuhakikisha   mapadri wana nyumba ya kuishi.

“Hivi sasa wa kwetu anakaa Dodoma mjini. Kwa hiyo tuna kazi ya kukarabati kanisa  lakini kwanza tukamilishe ujenzi wa nyumba ya mapadri,” alisema Pinda

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles