22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ataka kasi ujenzi wa mahakama

Mwandishi wetu -Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa uongozi wa mahakama nchini uhakikishe unakamilisha ujenzi wa miundombinu ya mahakama ili kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa katika kutafuta haki zao.

Akizindua Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa, Majaliwa alisema kati ya wilaya 139 za Tanzania Bara, 111 ndizo zenye mahakama za wilaya na nyingine 28 zinahudumiwa na mahakama za wilaya za jirani.

Alisema ni vema uongozi wa mahakama uhakikishe yale yote waliyojipangia kwenye mpango wao wa miaka mitano wa maendeleo ya miundombinu ya mahakama 2016/17 – 2020/21 unatekelezwa kwa wakati.

Majaliwa alisema kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Wilaya Ruangwa mwaka 2009, wananchi wa wilaya hiyo walilazimika kusafiri kilomita 180 kufuata huduma za mahakama wilayani Lindi.

 “Umbali huo mrefu ulisababisha wananchi wengi kupoteza muda mwingi ambao wangeutumia kwa shughuli za uzalishaji mali.  

“Wakati mwingine wananchi hao walikosa haki zao kwa kushindwa kumudu gharama za usafiri kuhudhuria mashauri yao wilayani Lindi,” alisema Majaliwa.

Alisema mahakama ni muhimu katika kudumisha amani na kuleta maelewano ndani ya nchi au jamii ambayo huwa ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi, hivyo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuamua kujenga mahakama hiyo wilayani Ruangwa pamoja na sehemu nyingine nchini.

Amesema kupitia mahakama, migogoro mingi hupata usuluhishi na hivyo kuimarisha hali ya amani na utulivu.

  “Kwa lugha nyingine, mahakama inapokuwa imara taifa letu huvutia uwekezaji kwa kuwa wawekezaji wanakuwa na uhakika na usalama wao pamoja na mali zao,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na mahakama kuhakikisha kuwa mipango yake iliyojiwekea inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, kwani bado kuna kazi kubwa mbele yao.

Wakati huo huo, Majaliwa aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kukusanya mapato kupitia mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji maduhuli ya Serikali (Government electronic Payment Gateway – GePG) kwani Serikali ilielekeza kila taasisi itumie mfumo huo ili kupunguza mianya ya rushwa na upotevu wa fedha.

Alisema amefurahi kusikia kuwa kwa kutumia mfumo wa GePG, mahakama iliweza kuongeza kiwango cha makusanyo kutoka Sh bilioni 1.6 mwaka 2017 hadi Sh bilioni 2.5 Desemba mwaka jana baada ya kuanza kutumia GePG.

“Fedha hizi zitatumika kuchangia ujenzi wa mahakama na miundombinu mingine ya kiuchumi unaoendelea katika kila kona nchini.

“Ni ukweli usiofichika kwamba hata wananchi nao wanafarijika kuona kuwa kile mnachowatoza kinaenda moja kwa moja kwenye mfuko mkuu wa Serikali, na baadaye kiasi fulani kinarudi kwenu kujenga miundombinu ya kisasa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, alisema kwa muda mrefu, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba na uchakavu wa majengo katika ngazi zote za mahakama, yaani mahakama za mwanzo, wilaya, hakimu mkazi, mahakama kuu na rufani.

Alisema ili kukabiliana na ukubwa wa changamoto ya upungufu na uchakavu wa majengo yake, Mahakama ya Tanzania ilitayarisha Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu (2016-2021).

“Mpango huu umetathmini hali ya majengo ya mahakama katika mikoa na wilaya zote za Tanzania Bara,” alisema Profesa Juma.

Alisema mpango huo umelenga kupunguza au kuondoa kabisa uhaba na uchakavu.

Profesa Juma alisema jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa ni kielelezo cha utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama ya Tanzania.

Pia ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa watumishi wa mahakama, kwamba majengo hayo ya kisasa na miundombinu bora, iambatane na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Kila mtumishi wa mahakama (kama walivyo watumishi wote wa umma) anao mkataba na watumiaji wa huduma za mahakama.

“Kipimo chetu cha kutimiza masharti ya mkataba huu, ni nguzo ya pili ya mpango mkakati wa mahakama ambayo ni ‘Upatikanaji na Utoaji wa Haki kwa Wakati’.

“Hivyo siku zote watumishi wa mahakama tukumbuke kuwa mahakama hii ni mali ya wananchi na wananchi wana haki ya msingi ya kupata huduma iliyo bora kwa wakati,” alisema Profesa Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles