Na Mwandishi Wetu, Songwe
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Eliseyi Mgoyi na maofisa wengine watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia amemwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe, Damian Sutta kuwakamata na kuanza kuwachunguza haraka maofisa hao, kisha ampelekee taarifa ofisini kwake.
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi maofisa hao jana, wakati alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa.
Maofisa wengine, waliosimamishwa kazi ni Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, Simon Noel, Bahati Chomoka ambaye ni mhasibu na Remmy Haule ambaye ni Ofisa Ugavi.
Waziri Mkuu, alisema maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya Serikali kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na wala hazifanyi shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki.
Alisema Kampuni ya Umbwila, ni moja kati ya kampuni zinazolipwa fedha nyingi za utengenezaji wa magari ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, huku ikiwa haina sifa za kufanya kazi hiyo.Kampuni zingine ni Julius Diesel, Kasaba na Mtoni Garage.
“Mfano duka la Umbwila ambalo linauza vipuri vya magari…halmashauri inalilipa fedha kwa ajili ya utengenezaji wa magari jambo ambalo si sahihi kwa sababu, lile ni duka la vipuri na si gereji. Wanamlipa muuza vipuri kama mtengeneza magari.
“Hatuwezi kuendesha Serikali kwa namna ambayo haikubaliki, watu tuliowapa dhamana ndiyo wanaongoza kwa vitendo vya rushwa na ufisadi. Wameifanya halmashauri hii kama shamba la bibi.”
Kutokana na hali hiyo, amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Eric Ambakisye kuhakikisha anasimamia vizuri utendaji ndani ya halmashauri.
“Halmashauri inanuka rushwa, tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona zingine zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali hii hapana, hatuhitaji rushwa wala harufu ya ufisadi,”alisema.
Amewataka madiwani na wakuu wa idara katika halmashauri zote, wabadilike na wahakikisha wanashirikiana kufanya kazi kwa ushirikiano.