Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema salfa iliyoingizwa nchini katika makontena 211 haina kasoro na inafaa kwa matumizi ya kupulizia mikorosho.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana alipozungumza na wajumbe wa kamati maalumu, waagizaji wa salfa na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) katika kikao alichokiitisha katika makazi yake ya Oysterbay, Dar es Salaam.
“Bodi kaandaeni taratibu za kawaida kusambaza salfa kwa wakulima ili waanze kupuliza dawa hiyo. Wasichelewe kupuliza kwa sababu msimu umeshaanza,” alisema.
Juni 4, mwaka huu, Majaliwa alimwagiza Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele, afanye uchunguzi wa mzigo wa salfa ulioko Bandari ya Dar es Salaam baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ripoti ya Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) kuwa salfa iliyoingizwa nchini na Kampuni ya ETG Inputs Ltd kwa niaba ya CBT haijakidhi viwango.
Majaliwa alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa kuna mkanganyiko miongoni mwa wakulima kuhusu matumizi ya kiuatilifu hicho licha ya Serikali kupokea taarifa ya CBT, ya kampuni iliyotengeneza salfa hiyo na iliyoletwa na mwigizaji aliyethibitishwa na kampuni tatu za kimataifa ambazo ni InterTech, Bureau Veritas na SGS.
Akitoa taarifa ya uchunguzi huo kwa Majaliwa, Profesa Manyele alisema walifanya uchunguzi katika makontena 21 ambayo ni sawa na asilimia 10 ya makontena yote 211 ili kubaini ubora wake.
“Uchunguzi ulifanyika kwenye maeneo ya purity, acidity na moisture contents kama ulivyokuwa umeelekeza. Sampuli zilichukuliwa kutoka Galco Inland Container Depot iliyoko Chang’ombe ambako ndiko mzigo wa salfa ulioletwa na Kampuni ya ETG Inputs Ltd unahifadhiwa,” alisema na kuongeza:
“Kwa kuzingatia matokeo ya kiuchunguzi wa kimaabara uliofanyika, viwango vilivyowekwa ndani ya mkataba na viwango vya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuhusiana na kiuatilifu cha salfa ni maoni yetu kuwa mzigo wa salfa ulioko ndani ya makasha 211 unakidhi viwango.”
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CBT, Maokola Majogo, alisema yeye na bodi yake watatekeleza maelekezo ya Majaliwa na akawataka wakulima wasisite kutumia salfa hiyo kwa sababu imeshathibitishwa na ofisi ya Mkemia Mkuu kwamba haina matatizo.
Kaimu Mkurugenzi wa CBT, Hassan Jarufu, alisema waliagiza salfa kwa kiwango kile kile cha mwaka jana kilichotumiwa na wakulima na kuleta matokeo mazuri.
“TPRI walichukua sampuli na kuleta majibu kuwa ina upungufu, kwa hiyo tukashindwa kuisambaza. Majaliwa alimwagiza Mkemia Mkuu afanye uchunguzi wake na sisi tumefurahia matokeo na tunaenda kutekeleza maelekezo yake ya kututaka tusambaze salfa kwa wakulima,” alisema.