33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa apigilia msumari marufuku sukari Zanzibar kuagizwa nje

Ramadhani Hassan – Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema anaamini Watanzania walimwelewa wakati akitoa maagizo katika Kiwanda cha Sukari cha Mahonda Visiwani Zanzibar, alipotaka sukari kutoka nje ipigwe marufuku.

Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni jana, Majaliwa alisema; “mimi naamini, Watanzania walinielewa na Watanzania hawa hata wenzangu wa Zanzibar, kwamba nilichosema ni sahihi, hao wanaotamka kwamba wamechefuliwa ni wanunuzi na sio Wazanzibar.

“Sera yetu ni moja ya kuwalinda Watanzania na tutawalinda na tutaendelea kufanya hivyo na tutakuwa wakali pale ambako mambo hayaendi,” alisema Majaliwa.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub (CCM) ambaye alidai kama kuna kitu kilimvutia ni ziara ya Waziri Mkuu Zanzibar na maagizo aliyotoa akiwa katika Kiwanda cha Sukari cha Mahonda.

 “Yale maagizo uliyotoa Waziri Mkuu ni sawa sawa na maagizo ambayo yangetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Sukari inunuliwe ya pale ikiisha ndio iagizwe nje, kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba, wewe ndio mwenye nyumba, zile kelele ulizozikuta pale zisikuumize. Soko kubwa la walaji liko Tanzania Bara.

“Je, ni lini mtafikiria angalau ile bidhaa kama zinavyotoka hapa kama saruji kutoka Tanga Cement, Twiga, Dangote na mabati kwenda soko dogo la Zanzibar angalao bidhaa zipatikane katika soko lile?” aliuliza Jaku.

Majaliwa akijibu, alisema wakati Serikali inahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini, ni lazima wawekezaji wa ndani walindwe kwa nguvu zote.

“Kama tani 36,000 ndio mahitaji ya eneo, kwanza tani 6,000 zingetoka na wale waagizaji basi wangepewa masharti ya kununua sukari ya ndani halafu unawapa kibali cha kuweka ‘top up’, lakini wanapoagiza sukari ya nje inakuja ndani haiwezekani.

“Mimi kama Waziri Mkuu mwenye wajibu hata kwa chama changu kufuatilia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi, mimi kwa pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ndio wenye jukumu la kufuatilia utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Suala la viwanda liko kwenye ilani ya CCM na ninapaswa kwenda kokote Tanzania kufuatilia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi na sina mipaka, sasa leo napokuta mahali ilani haitekelezeki, lazima niwe mchungu na nitaendelea kuwa mchungu.

“Lazima tuweke mpango wa kuwalinda wawekezaji wa ndani kwa kuwahakikishia soko na masoko tunayo. Pale naambiwa waagizaji wako watatu, kwa nini usiwape masharti angalao rahisi. Lakini unaagiza zote kutoka nje halafu huyu atauza wapi? Haiwezekani, haiwezekani. Halafu mtu anasema nimewachefua Wazanzibari. Nimewachefua Wazanzibar au nimewachefua wanunuzi? Mheshimiwa Spika kwenye hili inabidi nilieleze zaidi.

“Kile kiwanda pale Mahonda kinawanufaisha wale wananchi wa Kaskazini Unguja kwa sababu wenyewe wanalima miwa na soko lao ni kile kiwanda, ukichukua sukari ya nje kama vile, miwa wanayolima haiwezi kupata soko muda wowote na ni kuwaumiza Wazanzibar.

“Kile kiwanda kiko pale kinaajiri watumishi 400 na wanufaika ni wale walioko Kaskazini Unguja, lakini leo usipouza, huyu hawezi kuajiri na hawezi kulipa mishahara kwa sababu sukari iko ghalani, haiwezekani kwa sababu kiwanda kiko pale kinalipa kodi na kodi ndiyo hiyo ambayo imeniwezesha kwenda kuona kituo cha afya kule Bambi, kituo cha afya kule Kizimkazi, nimeona maabara nzuri imejengwa yenye viwango pale Gwajuu, nimeenda pia Unguja na Kaskazini Pemba nimekuta Veta inajengwa nzuri kwa sababu ya fedha ya kodi ya viwanda, haiwezekani,” alisema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles