RAMAADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa onyo kwa maofisa elimu nchini kutojihusisha kwenye vitendo vya kupanga na kuiba mitihani ya Taifa.
Onyo hilo alilitoa jijini hapa jana alipofungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Umoja wa Maofisa Elimu Mikoa na Wilaya nchini.
Alisema wapo baadhi ya walimu wanaoshirikiana na maofisa elimu kuiba mitihani jambo ambalo ni baya na kuwataka waache mara moja.
“Ninatoa onyo kali kwa baadhi yenu wanaojihusisha na wizi, udanganyifu na uvujaji mitihani. Tabia na mwenendo huu unalivunjia heshima na hadhi taifa letu,” alisema.
Waziri Mkuu alisema serikali haitamsamehe yeyote atakayebainika kwenye wizi huo na hatua kali za sheria zitachukuliwa.
Vilevile aliziagiza kamati za mitihani za mikoa na wilaya kusimamia sheria, kanuni na taratibu bila uwoga, upendeleo na kutoyumbishwa.
Alisema kwa watakaobainika hatua kali za nidhamu na utumishi zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria, taratibu na miongozo inayotolewa.
Majaliwa pia aliwataka maofisa elimu nchini kusimamia nidhamu na mienendo ya wanafunzi.
“Hili tatizo la nidhamu mbaya kwa wanafunzi ni jukumu la walimu wote wanatakiwa kutekeleza majukumu yao ya kufundisha, kulea, kuwaongoza na kuwaendeleza wanafunzi kwa mwili.
“Serikali imesikitishwa na matukio ya hivi karibuni ya athari ya viboko kwa wanafunzi shuleni ikiwamo kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu pamoja na tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kuna udhaifu katika utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni.
Hivyo aliwakumbusha maofisa elimu kuwakumbusha walimu kuzingatia mwongozo wa kutoa adhabu shuleni chini ya kifungu cha 61 cha Sheria ya Elimu sura 353 pamoja na kanuni zake.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema wizara yake na TAMISEMI zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu zaidi katika kutatua changamoto mbalimbali za utaalamu na taaluma.
Pia aliwataka maofisa elimu kutoa taarifa na takwimu sahihi kuhusu elimu ziweze kutumika kwenye mipango mbalimbali ya elimu badala ya kuzipika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo, aliwaagiza maofisa elimu kusimamia fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu.