27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aonya wadaiwa sugu NSSF

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Na ELIYA MBONEA, ARUSHA

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) limejipanga kufanya mageuzi makubwa ya uwekezaji katika sekta ya viwanda utakaoinua viwango vya ajira na kuboresha maisha ya wanachama.

Mikakati hiyo imelenga kuitikia wito wa Rais Dk. John Magufuli wa kuijenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama suluhisho la kuwakwamua Watanzania kwa kuongeza ajira.

Hayo yalielezwa jana kwenye mkutano wa sita wa wadau wa NSSF uliofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Akifungua mkutano huo mjini hapa jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Serikali inataka kuleta maendeleo kwa kuhakikisha unakuwapo  uchumi wa kati wenye kujengwa na viwanda.

Waziri Mkuu alisema anafarijika kuona NSSF ikiwa imedhamiria kwenda na mwelekeo huo kwa kupanua wigo wa uwekezaji na kuelekea katika viwanda hatua itakayoongeza ajira na kukuza uzalishaji nchini.

“Uamuzi huu utawawezesha NSSF na mifuko mingine kupata wanachama wapya na kukusanya michango zaidi na kuiwekeza   kutimiza lengo la msingi la hifadhi ya jamii.

“Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana kukabiliana na tatizo la sukari nchini kwa kuamua kujenga kiwanda cha sukari eneo la Mkulazi mkoani Morogoro kitakachotoa  tani 200,000 kwa mwaka.

“Lakini, pia kiwanda hicho kitatoa ajira zaidi ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mifuko hiyo. Huu ni moyo wa uzalendo unaofaa kuigwa na kila mtu, taasisi na kampuni mbalimbali,” alisema na kuongeza:

“Kazi ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza kufanywa kwa namna mbili, kwanza ni kwa kuvifufua vilivyopo na pili ni kwa kuanzisha viwanda vipya na kwa NSSF wao wameweza kutekeleza yote mawili.

“Mbali na ujenzi wa kiwanda hicho cha sukari, NSSF pia imeanza kazi ya uwekezaji wa kutoa mikopo kwa viwanda nchini kwa dhamira hiyo hiyo ya kuijenga Tanzania yenye viwanda.

“Nimeelezwa hapa kwamba NSSF imetoa mkopo wa Sh bilioni 3.1 za kukuza uzalishaji wa viuatilifu katika kiwanda kilichopo Kibaha, lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji.

“Natoa rai kwa taasisi zilizonufaika au zitakazonufaika na mikopo hii kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na pia kurejesha kwa wakati kwa mujibu wa mikataba   wengine nao wanufaike,”

Kuhusu suala la baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati na kusababisha usumbufu kwa wanachama, Majaliwa alisema suala hilo halikubaliki hivyo aliwataka waajiri wote nchini kuheshimu sheria na kuwasilisha michango hiyo kwa wakati.

Kwa waajiri wanaodaiwa na NSSF, alimuagiza mkurugenzi mkuu kuwaandikia barua za kutaka wawasilishe fedha wanazodaiwa mara moja na wale ambao hawatalipa ndani ya muda watakaopangiwa, wafikishwe mahakamani.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu aliwajulisha wadau wa NSSF kuwa Serikali imelipa Sh bilioni 722.7 kati ya madeni ya michango ya Sh bilioni 964.2.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Professa Godius Kahyarara, alisema NSSF imejipanga kuona viwanda vya ndani vikizalisha bidhaa za matumizi ya ndani na kuziuza katika soko la nje kupata fedha za kigeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles