24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aongoza maelfu kuaga

Upendo Mosha-Moshi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wananchi katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, huku akifikisha salamu za Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza wakati akitoa salamu za Serikali, Majaliwa alisema kifo cha Dk. Mengi kimekuwa ni pigo kwa Serikali kutokana na mchango wake wa kiuchumi.

Majaliwa alisema kifo cha Dk. Mengi ni pigo kubwa na Serikali itaendelea kuyaenzi yote aliyoyatenda katika taifa.

Alisema Dk. Mengi amewaachia funzo, hasa kwa wafanyabiashara, namna ya kuishi na kuwatunza watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo masikini.

“Tutamkumbuka Dk. Mengi katika mambo mengi na yapo mengi ya kujifunza kwake, tutayaishi maisha yake,” alisema.

Mbali na hilo, Majaliwa aliitaka familia kuendeleza miradi yote ya maendeleo ambayo ilikuwa kwenye mpango na ndoto za Dk. Mengi.

“Dk. Mengi alikuwa na mipango mingi, naomba familia muweze kuyatimiza kwa kuyaendeleza, miongoni mwa mambo tutamkumbuka ni kuchangia uchumi wa taifa letu,” alisema.

WASIFU WA MAREHEMU

Mtoto wa marehemu, Abdiel Mengi akisoma risala kwa niaba ya familia, alisema baba yake alikuwa na sifa kuu tatu ambazo ni uzalendo, ubunifu au ujuzi wa mambo na kwamba alikuwa ni mtu asiyekata tamaa.

“Baba alifanyika baraka kwa watu wote na jamii yote ya Tanzania na nje ya nchi, yeye alikuwa na sifa kuu tatu, moja wapo ni uzalendo. Aliipenda nchi yake jambo lililomfanya kupenda kujitoa,” alisema.

Alisema Dk. Mengi alikuwa ni mtu wa kipekee kwani alikuwa mbunifu na mjuzi katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na aliona fursa mapema na kuzifanyia kazi kabla ya mwingine.

“Baba alikuwa ni mtu imara na mtu mjuzi na mwenye maamuzi, hakuwa dhahifu na alikuwa akifanya mambo mengi lakini yale muhimu, ikiwemo kugusa sekta zote ikiwemo walemavu, mazingira na kuhubiri amani na utulivu wa nchi,” alisema.

Alisema sifa kuu ya tatu, Dk. Mengi alikuwa ni mtu anayependa kuvunja mipaka na pale dunia ilipokuwa ikimtazama na kusema yeye ni mtoto wa masikini na atakufa masikini hakukubali, bali alipambana na kujinasua kutoka katika hali hiyo.

“Baba alikuwa mtu wa kuvunja mipaka kwani dunia ilisema yeye ni masikini na atakufa masikini, lakini hakukubali na hata alipofanikiwa, dunia ilimwambia yeye ni tajiri na hawezi kuchangamana na masikini, lakini alikataa hali hiyo na kuwasaidia na masikini na kula nao,” alisema.

Mbali na hilo alitoa shukrani zake za dhati kwa viongozi wa Serikali, wananchi na viongozi wa dini walioshiriki katika kipindi chote tangu walipopatwa na msiba Mei 2, mwaka huu.

SALAMU ZA KENYATTA

Akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Nyokabi Kenyatta ambaye ni dada wa kiongozi huyo, alisema Mengi alikuwa ni miongoni mwa wafanyabiashara ambao walijitoa kwa hali na mali kuwasaidia wale waliokuwa na shida.

Alisema Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye aliweza kujitoa kwa mali na fedha zake katika kuhudumia wanyonge.

“Taifa la Kenya linasikitika sana na msiba huu kwani Mengi ni miongoni mwa wafanyabiashara wachache ambao walikuwa tayari kujitoa kwa Waafrika wenzake, Tanzania imepata pigo sana na Afrika kwa ujumla, mliobaki ikiwemo wafanyabiashara myaishi yale mema aliyokuwa akiyatenda,” alisema.

MBOWE

Naye Freema Mbowe, alisema Dk. Mengi alikuwa akiishi maisha ya kawaida licha ya kuwa tajiri.

Alisema Dk. Mengi alikuwa mtu mwenye upendo na kuwa mwenye uwezo mkubwa kiuchumi, hakuwa mtu mwenye kiburi bali alitumia utajiri wake kusaidia watu mbalimbali katika jamii.

“Mengi alikuwa mtu wa tofauti sana kwani pamoja na utajiri aliokuwa nao, haukumpa kiburi bali alikuwa mnyenyekevu na kauli zake zililenga kujenga, kupatanisha na hakuwa mtu wa kukata tamaa.

“Kuna vitu viwili hapa duniani ambavyo mtu asipovitumia vizuri vinaleta kiburi kama visipotumika kwa unyenyekevu, navyo ni madaraka na utajiri, Mengi utajiri wake haukumpa kiburi,” alisema.

Mbowe alisema Dk. Mengi hakuwa kiongozi wa kisiasa bali alitumia muda mwingi kuitumikia jamii kwa mali na fedha zake na jamii inapaswa kuyaenzi yote ambayo amekuwa akiyafanya.

NDUGAI ATOA SALAMU

Akitoa salamu zake, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwataka Watanzania kutoamini kila kinachoandikwa na mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikifanya upotoshaji wa baadhi ya mambo ya kitaifa, Bunge na hata hadhi za viongozi wa kisiasa na Serikali kwa ujumla.

Aliwataka Watanzania kuwa wepesi kuhoji ukweli wa baadhi ya mambo yanayoandikwa katika mitandao ya kijamii na kwingineko ambako kumekuwa na nia ovu ya kupotosha jamii.

“Kama Bunge tunamkumbuka Dk. Mengi ambaye alitusaidia kwa kuwapo kwa vyombo vingi vya habari, makampuni mbalimbali ambayo yametoa ajira kwa Watanzania ambacho ni kilio cha wananchi wengi,” alisema.

WAFURIKA KUUGA MWILI WA DK. MENGI

Licha ya kuwapo kwa manyunyu ya mvua, bado maelfu ya wakazi wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga waliendelea kuwepo katika msururu wenye urefu wa takribani mita 200 kwenda kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Dk. Mengi.

Wananchi hao ambao walikuwa wamegubikwa na majonzi, wakiwa wa kada zote, wakiwemo walemavu, wengine walishindwa kujizuia na kuangua vilio wakiwa katika misitari ya kwenda kutoa heshima za mwisho.

Hata hivyo kulikuwapo na changamoto kwenye lango kuu la kuingia katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Usharika wa Moshi Mjini.

Miongoni mwa changamoto ni pamoja na vijana wa skauti waliopewa jukumu la kusimamia utaratibu wa watu kuingia kushindwa kuhimili wingi wao na kulazimu Jeshi la Polisi kuongeza askari kuimarisha ulinzi.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikundi vingine vya ulinzi walilazimika kufunga geti hilo na kuruhusu watu kuingia kwa utaratibu wa mistari ambao uliharakisha utoaji heshima za mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles