30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Majaliwa akaribisha Wavietnam kununua korosho, kujenga viwanda

Mwandishi wetu-Dar es salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini, Nguyen Doanh, na kuwakaribisha wafanyabiashara kutoka nchi hiyo kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya viwanda.

Alisema Rais Dk. John Magufuli ameanzisha Wizara ya Uwekezaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuifanya Tanzania kuwa mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

 Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana  ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni Dar es salaam, aliwaalika wawekezaji katika sekta ya viwanda hususani vile vinavyotumia malighafi za mazao ya kilimo yanayolimwa nchini.

 “Serikali imeendelea kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kuendesha biashara kwa kupitia upya sheria, kanuni na taratibu za biashara na kuzifuta zile ambazo zimethibitika kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji kuwa magumu,” alisema.

Alisema nchi ya Vietnam imepiga hatua katika ujenzi na uendeshaji wa viwanda vya nguo, Tanzania ingefurahi kuona kwamba viwanda vya aina hiyo vinajengwa hapa nchini na wawekezaji kutoka nchi hiyo.

Akizungumzia kuhusu soko la korosho, Majaliwa alisema Tanzania ina korosho za kutosha na inawakaribisha wafanyabiashara kutoka Vietnam waje kuzinunua.

“Kwa wale wenye uwezo wa kujenga viwanda vya kuchakata korosho nao amewakaribisha na kuahidi kuwa Serikali iko tayari wakati wote kuwasaidia,” alisema. 

Balozi Doanh, alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu juu ya ujio wa Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung anayetarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini kuanzia Julai 9 hadi 11. 

Alisema Naibu Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kuambatana na wafanyabiashara wasiopungua 20 kutoka kampuni kubwa za Vietnam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,184FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles