27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa akaribisha wawekezaji toka Mauritius

MWANDISHI MAALUMU – Yokohama, JAPAN

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Mauritius waje washirikiane na Watanzania katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya utalii, viwanda vya sukari, nguo na bidhaa za uvuvi.

Ametoa kauli hiyo jana alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar katika Ukumbi wa Monyesho wa Pasfico, Yokohama nchini Japan.

Alisema nchi ya Mauritius ina uwezo mkubwa katika uzalishaji wa sukari na wanayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Watanzania katika kilimo cha miwa na ujenzi wa viwanda vya sukari.

Majaliwa alisema Tanzania ina ardhi nzuri na kubwa inayofaa kwa kilimo cha miwa pamoja na soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Alisema uwekezaji katika sekta ya sukari utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli za kuhakikisha inamaliza tatizo la upungufu wa sukari nchini.

Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii, Waziri Mkuu alisema Mauritius imefanya vizuri sana katika utalii na hasa ule wa kutumia fukwe za bahari.

“Kwa vile Tanzania inazo fukwe za bahari na maziwa naamini ushirkiano katika eneo hilo utatuletea tija,” alisema.

Kuhusu usafiri wa anga, Waziri Mkuu alisema kuwa wakati  umefika sasa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanza safari za kwenda Mauritius ili kuvutia watalii wengi wanaokwenda huko  kufanya utalii wa fukweni waje  pia nchini.

Kuhusu viwanda vya nguo, Waziri Mkuu aliwahamasisha wafanyabiashara wa Mauritius kuwekeza nchini hasa katika viwanda vya nyuzi za pamba na nguo kwani Tanzania hivi sasa inazalisha pamba nyingi na yenye ubora wa juu.

Kadhalika, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu sekta ya Uvuvi akisema Tanzania ina eneo kubwa la bahari na maziwa linalofaa kwa uvuvi wa kibiashara na lina samaki wengi, lakini wanavuliwa kwa kiwango kidogo kutokana na uwekezaji duni katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo na wizara na taasisi zinazohusika na masuala ya uwekezaji nchini  ili kupata taarifa za kutosha zitakazomwezesha kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi yake waje wawekeze nchini.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi na viongozi kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles