Mwandishi wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kutafuta mbinu bora zaidi na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili.
Ametoa tamko hilo leo, Jumatano, Julai 17, alipokuwa akifungua maonesho ya 14 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, ambayo yatafungwa Julai 20, mwaka huu.
“Tume itafute mbinu bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili. Ni wakati muafaka kwa Tume kujipambanua kwenye uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kwamba kazi kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kuvisaidia kutatua changamoto zinazovikabili,” amesema.
“Naomba nieleweke vizuri kwamba hakuna mbadala wa elimu bora bali nasisitiza tume ivisaidie vyuo vikuu kufikia viwango vinavyotakiwa na siyo kuwapunguzia viwango vya matakwa ya usajili,” amesema.
Aidha amesema matarajio ya serikali ni kuona tafiti na vipimo vya ufanisi kwenye vyuo vikuu viwe ni kiasi gani vyuo hivyo vinatoa bidhaa mbalimbali za kuleta ajira pamoja na kukabiliana na matatizo ya kijamii.
“Ningefurahi iwapo kuanzia sasa kipimo cha ufanisi wa vyuo vikuu vyetu iwe katika kupima jitihada za vyuo vyetu kuisaidia Serikali katika azma yake ya kufikia kwenye uchumi wa kati,” amesema.