30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aeleza maofisa TRA walionyimwa rushwa walivyomtesa mfanyabiashara

Na Mwandishi wetu

MAOFISA watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wameingia matatani baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kueleza walivyofungia kwa miaka mitatu mzigo wa mfanyabiashara aliyekataa kuwapa rushwa.

Baada ya Majaliwa kueleza hayo katika mkutano wa wafanyabiashara na Rais John Magufuli, kiongozi huyo wa nchi alimuagiza Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, kuwasimamisha kazi na kumfidia mfanyabiashara huyo kwa hasara aliyopata.

Pia aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata maofisa hao na kuwafikisha mahamani.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Majaliwa alisema mfanyabiashara huyo alikamatwa mwaka 2015 na mzigo wake kufungiwa na maofisa hao mpaka Aprili mwaka huu ambapo ulitolewa baada ya yeye kuingilia suala hilo.

 “TRA wamekuwa wakilalamikiwa sana yupo mfanyabiashara moja alikamatwa mwaka 2015 akaombwa rushwa akakataa kutoa na akakubali mzigo ukae huko lakini hayuko tayari atoe rushwa,” alisema.

Alisema mfanyabiashara huyo alitoa mzigo wake Zambia na maeneo yote alipita bila tatizo mpaka alipofika Dar es Salaam ndipo maofisa hao walipomkamata wakamtaka atoe rushwa.

“Usiku ule wakamsindikiza mpaka Kariakoo, akaingia ndani akasema hatoki wakitaka wamuue, baadaye wakampeleka kwenye bohari yao, akauacha mzigo ukakaa miaka mitatu sasa ndio Aprili mwaka huu tukaagiza arudishiwe mzigo wake,”alisema.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli aliingia kati akimhoji Majaliwa kuwa hao waliomwonea wafanyabiashara kama  wapo.

Baadaye Kamishna wa TRA, Charles Kicheere alisema atamkabidhi kuwa maofisa hao wapo.  

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alimwagiza Mkurugenzi wa Takukuru, kuwakamata maofisa hao watatu wa TRA na kupelekwa mahakamani huku akimtaka Kicheera kuwasimamisha kazi.

Pia aliitaka TRA kupiga hesabu ya hasara ambayo mfanyabiashara huyo aliipata katika kipindi hicho cha miaka mitatu na wamfidie.

 Majaliwa pia alisema akiwa kwenye mkutano huo mfanyabiashara mmoja amemwandikia ujumbe kwenye karatasi akimwelekza namna TRA walivyo miungu watu.

“Mmoja kaniandikia kuwa wafanyabiashara wengi wanaogopa kusema ukweli kuhusu TRA kwa sababu wanaogopa kushushughulikiwa.

“Kaniandikia ‘fuatalia utaamini TRA ni miungu watu wanakuadhibu kwa kodi kubwa halafu wanataka na rushwa, ukishindwa duka linafungwa halafu wanasema maagizo kutoka juu’” majaliwa alimukuu ujumbe alioandikiwa.

Katika hatua nyingine alisema Serikali imeanza kuyafanyia kazi maeneo yanayogusa biashara katika sekta zote.

 “Tumeenda pia viwandani kusikia nini changamoto za sekta hiyo, umoja wa wauza bodaboda kusikia kero yao ni nini, sekta ya utalii lakini hata huku serikalini tumekutana TFDA, TBS, GSI, TIC hata mkemia mkuu.

“Kazi hii imetufanya tubaini kuwa ni kweli tuna tozo nyingi zinazofanana, tumekutana mawaziri mwezi uliopita kila mmoja apitie kila tozo zinazofanana ili kuacha tozo moja kwa taasisi moja.

“Taasisi hizi nazo zinajirudia mfano TBS, TFDA na Mkemia Mkuuu wa Serikali, hivi vitu vinafafa kwanini tusiwe na taasisi moja strong inayosimamia haya?

“Tumepelekea haya kwa AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) ili atoke na muswada unaojulikana business facility act ili tuachane na usumbufu uliopo pia mlipe kodi sahihi. 

“Malalamiko yenu makubwa ni TRA, Kamishna Mkuu wa TRA hakuna haja ya waziri hata wewe usimamie changamoto zilizotolewa, tuna tatizo la kufunga maduka ya watu bila sasa. Kuna timu nyingi ambayo inakusanya kodi hatuna uhakika kama zinaundwa na TRA yenyewe halafu wanasema timu kutoka juu…juu wapi,”alihoji Majaliwa.

Alisema malalamiko yote yaliyotolewa na wafanyabiashara hao watayafanyia kazi na nia ya Serikali ni kulinda bidhaa za ndani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles