29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aeleza madini yanavyochangia pato la Taifa

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,  amesema hatua iliyofikiwa ya kuzuia uvunaji haramu wa rasilimali kwa utaoji wa cheti cha uhalisia kwa madini ya bati, kutaiwezesha sekta ya madini nchini kuchangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020 kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli. 

Pamoja na hilo Waziri Mkuu amezindua utoaji wa cheti cha uhalisia  kwa madini ya bati kitakachokuwa kinatolewa na Tanzania, ambapo alisema cheti hicho ni muhimu kwa Taifa letu na nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maziwa Makuu kwa kuwa kitaweka utaratibu wa kudhibiti madini hayo.

Alisema mambo waliyojifunza katika mkutano huo yatasaidia kuongeza kasi ya kukua kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa. 

“Wizara ya Madini shirikianeni na wadau wengine katika kuhakikisha mkutano huu unaendelea kuboreshwa kila mwaka na kuongeza washiriki ili kupanua uelewa wa pamoja,” alisema  

Waziri Mkuu  alisema kuwa matarajio ya kila mmoja wao kwamba uzinduzi huo walioufanya utasaidia katika kutekeleza Itifaki ya Kuzuia Uvunaji Haramu wa Rasilimali yaani.

“…nafahamu kwamba mkutano wa aina hii unaoihusu sekta ya madini unafanyika kwa mara ya pili hapa nchini. Nitoe wito kwa nchi wananchama kuhakikisha mikutano ya aina hii iweze kuandaliwa katika nchi nyingine na iwe endelevu katika kutoa fursa kwa wadau kutambua fursa zilizopo nchi nyingine,” alisema  

Alisema Serikali inaridhishwa na kuimarika kwa utendaji kazi wa sekta ya madini nchini kutokana na mafanikio yake ikiwemo kuongezeka kwa mchango wake katika pato la Taifa. 

“Mathalan, kupitia Taarifa ya Hali ya uchumi ya Mwaka 2019, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020, mchango wa Sekta ya Madini ulikua kwa asilimia 13.7,” alisema 

Alisema kwenye kipindi hicho, sekta ya madini ilikuwa ya pili katika kuchangia pato la Taifa ikitanguliwa na sekta ya ujenzi ambayo ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 16.5. 

“Katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya shilingi  bilioni 242.53 sawa na asilimia 51.5 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi  bilioni 470.89.Makusanyo hayo yalitokana na mrabaha, ada ya ukaguzi wa madini, huduma za kimaabara, mauzo ya machapisho mbalimbali ya kijiolojia na ada za leseni,” alisema 

Licha ya hali hiyo alisema kuwa kukabiliana na utoroshwaji wa madini, Serikali iliamua kuanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kuondoa mianya ya kuweza kufanya biashara ya madini kupitia njia zisizo rasmi. 

“Hadi sasa tuna jumla ya masoko ya madini 27 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 28 kote nchini,” alisema  

Alisema masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji sahihi wa takwimu za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwake, hivyo ametumia fursa hiyo kuwafahamisha wadau wa mkutano huo kuwa masoko hayo yapo wazi kwa wadau wa ndani na nje ya nchi. 

Awali, Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema mkutano huo umehudhuriwa na nchi 11 wanachama waJumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) pamoja na wadau wa sekta ya madini wa ndani na nje ya nchi.

Biteko alisema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa madini katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo wachimbaji, wanaotengeneza na kuuza tekinolojia, wadau wenye mitaji na wasionayo lakini pia kwa upande wa Serikali kujifunza namna ya kuboresha na kuifanya sekta ya madini kuwa ni sekta yenye kuongeza tija kwa Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles