23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aagiza Takukuru kushughulikia wanaotumia rushwa kusaka uongozi

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwashughulikia wanasiasa ambao wanatumia rushwa kusaka madaraka, huku akiwasihi wanasiasa kuacha kutumia rushwa kwenye kusaka nafasi za uongozi.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akifungua jengo la Intelejensia la Takukuru makao makuu mkoani Dodoma.

Majaliwa alisema kitendo cha wanasiasa kutumia rushwa kusaka nafasi mbalimbali za uongozi nchini kimekuwa kikirudisha  nyuma maendeleo.

Aidha, aliitaka Takukuru kuendelea kung’ata mafisadi popote walipo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua dhidi ya wote watakaobainika kushiriki kutoa ama kupokea  rushwa kwani sheria inawaruhusu kwenda moja kwa moja mahakamani.

 “Endeleeni kung’ata mafisadi kwa faida ya wananchi, nawasihi wanasiasa kuacha kutumia rushwa katika kugombea nafasi za uongozi, tutumie kauli za baba wa taifa, tunapotumia fedha kusaka uongozi utazirudisha vipi? Wananchi tunao wajibu wa kuchagua viongozi bora wenye maono watakaotuvusha,” alisema Majaliwa.

Alisema ufunguzi wa jengo hilo ni kielelezo tosha kuhusu juhudi za taasisi hiyo katika kukabiliana na rushwa nchini kwani litatumika katika kukusanya na kuchakata taarifa za rushwa, lakini zaidi kufanya kazi kwa ufanisi.

“Uzinduzi wa jengo hili ni kielelezo tosha juu ya juhudi za taasisi katika kukabiliana na rushwa nchini, litatumika katika kukusanya na kuchakata taarifa za rushwa, lakini zaidi kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema Majaliwa.

Alisema jitihada za Takukuru zimefanikiwa kudhibiti matumizi ya hovyo ya fedha za umma, lakini pia kuongeza mapato ya Serikali hatua ambayo imesaidia kurejesha imani ya wananchi kwa watumishi wa umma.

Majaliwa alisema baadhi ya mafanikio ya taasisi hiyo ni pamoja na kudhibiti na kurejesha fedha za vyama vya ushirika vya wakulima wa zao la korosho kwa mikoa ya Lindi na Mtwara na wakulima wa zao la pamba wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine nchini.

“Natoa pongezi kwa Takukuru katika kudhibiti na kurejesha fedha za vyama vya ushirika kote nchini, mfano katika mikoa ya Lindi na Mtwara na pamba kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine,” alisema Majaliwa.

Aliitaka Takukuru kutumia jengo hilo kukusanya na kuchakata  taarifa kama ambavyo imeonyesha kwa baadhi ya matukio nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema Kurugenzi ya Itelejensia ni muhimu kwa taasisi hiyo kwani itasaidia kuchakata mambo yaende haraka.

Alisema kwa sasa bado wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa majengo ya ofisi za intelejensia na alidai wamejipanga kuhakikisha kila mkoa na wilaya unakuwa na jengo lake.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema hivi karibuni  wanatarajia kufungua ofisi mpya katika wilaya za Ngorongoro, Masasi, Manyoni na Namtumbo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles