30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aagiza pasi za kusafiria za Wakandarasi zikamatwe

*Ni za Wakorea wanaojenga meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu

*Akagua daraja la Busisi-Kigongo, aagiza watumishi walipwe stahiki zao

Na Clara Matimo,Mwanza

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa kwa pasi za kusafiria za wataalamu wa kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini wanaojenga meli ya MV Mwanza Hapa kazi Tu jijini Mwanza hadi wakamilishe kazi yao.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Mei 7, 2022) wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa mkoa huo mara baada ya kukagua ujenzi wa meli hiyo katika eneo la Mwanza South, wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza.

“Nimemwagiza Afisa Uhamiaji wa Mkoa akamate pasi zao mara moja na ahakikishe hakuna mtu anatoka nje ya mkoa huu hadi hii kazi ikamilike. Nimeambiwa wako saba, lakini hapa wako watatu. Watafuteni hao wengine wako wapi,” amesema Majaliwa.

Wenye pasi hizo ni Mkurugenzi wa GAS Entek, Dong Myung Kwak, na wasaidizi wake, Kyunghan Choi na Kyuh Yun Kwak ambaye ni mtoto wa Mkurugenzi huyo.

“Nimeingia ndani kukagua kazi ya ujenzi lakini sijaridhika nayo. Katika maelezo yao nimebaini kuwa kampuni tuliyoingia nayo mkataba ya GAS Entec imeuza share zake bila Serikali kuarifiwa. Waliouziwa, walipokuja walishangaa kuona ujenzi wa meli kwa sababu suala la ujenzi liko nje ya mauziano yao,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mwanza kwa ziara ya siku moja, amesema Serikali imeshalipa asilimia 80 ya gharama za ujenzi wa meli hiyo lakini kazi iliyofanyika kwa mujibu wa mkataba ni asilimia 65 tu. Amesema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa wafanyakazi walikuwa 118 lakini sasa wamebakia 22 tu.

“Haiwezekani tuwalipe hela hiyo, kazi haiendi kama ilivyopaswa. Tena wamepunguza Wafanyakazi kutoka 118 hadi 22, tunajuaje kama kesho watawaondoa hao 22 na wao wenyewe wapande ndege kurudi kwao, au waende Nairobi kupanda ndege,” amesema Majaliwa.

Amesema ameshawasiliana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ameridhia hatua hiyo. “Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia hatua hii.

“Hawa watu wasiondoke hadi kazi ikamilike na kama wataondoka basi  atakayewadhamini ni Balozi wao. Serikali tutaendelea kuwasiliana na Balozi wa Korea Kusini na tunaamini kazi hii itakamilika. Wizara husika simamieni na kuhakikisha kazi inakamilika kwa mujibu wa mkataba,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema hakuna mradi wa kimkakati ambao utakwama. “Mheshimiwa Rais ameagiza tusimamie hii miradi, nasi ndiyo maana tuko tuko barabarani kila siku Ninawaomba Watanzania muamini kuwa Serikali yenu iko imara. Na pia niwahakikishie viongozi wa Chama cha Mapinduzi mliopo hapa kwamba Ilani yetu itatekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90,” amesema.

Mapema, Mkurugenzi wa GAS Entek, Kwak alimweleza Waziri Mkuu kuwa amelazimika kupunguza wafanyakazi kwa sababu ana makontena matatu bandarini ambayo anataraji yataanza kutoka baada ya wiki mbili.

Kauli ya Kwak ilikanushwa na Meneja Mradi ambaye pia ni Mhandisi Mkazi, Lt. Col. Vitus Mapunda kwamba makontena matatu ni sehemu ndogo sana ya kazi iliyobakia na ambayo inatakiwa kuwa imefikiwa.

Gharama za ujenzi wa meli hiyo ni dola za Marekani milioni 39 sawa na Sh Bilioni 97 na itafanya safari zake katika nchi zote ambazo ziko ukanda wa ziwa Viktoria na ikikamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo.

Katika hatua nyingine, Majaliwa baada ya kukagua ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu alielekea kwenye eneo la Kigongo Busisi kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la JPM lenye urefu wa kilomita tatu.

Akiwa katika eneo hilo ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikutane na watendaji wa Idara ya Kazi mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha watumishi katika mradi huo wanalipwa stahiki zao ipasavyo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mbunge wa Sengerema, Hamisi Tabasamu aliyedai kuwa licha ya mradi huo kuendelea lakini watumishi wamepungua na wanakimbilia katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

“Mkandarasi aimarishe utendaji kazi ili ujenzi wa daraja hili ukamilike. Pia wananchi nawaomba mtoe ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi iendelee vizuri,” amesema.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Mhandisi Benjamin Michael alisema awali kulikuwa na wafanyakazi 813 na sasa wamebaki 744 baada ya wengine kuacha kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, alimuhakikishia Waziri Mkuu Majaliwa kwamba atasimamia miradi hiyo kwa ukamilifu na hakuna fedha ya serikali itakayoliwa na watumishi wacheche wasio waadilifu.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu kulikuwa na tabia kwamba mtua akiiba Kigoma anahamia Geita, tumekubaliana mtumishi yeyote anayekuja ndani ya mkoa huu tunapekua faili lake kama ni mwizi anarudi  alikotoka akabanwe kulekule hatutakubali mkoa huu uwe ni makimbilio ya wezi wa mali za umma,”alisema Mhandisi Gabriel.

Septemba 3, Mwaka 2018 serikali iliingia mkataba  wa ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi tu na kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini utakayogharimu jumla ya Sh bilioni 97 ikiwa ni mbadala wa meli ya MV Bukoba iliyozama mwaka 1996 na mradi huo unasimamiwa na Kampuni ya Huduma ya Meli nchini (MSL).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles