27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aagiza ofisa manunuzi, mzabuni Kinampanda wakamatwe

Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda kumkamata Ofisa Manunuzi wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, Francis Muyombo kwa kughushi nyaraka na kukiuka taratibu za manunuzi ya serikali. 

Pia amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike kumkamata na kumhoji aliyekuwa mzabuni wa chuo hicho, Joseph Kisaka kwa kuwapatia vifaa vilivyo chini ya kiwango. 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Jumapili Oktoba 6, wakati akikagua ukarabati wa majengo chuoni hapo ambapo pamoja na mambo mengine alibaini risiti ikionesha kitasa kimoja kimenunuliwa kwa Sh 70,000 badala ya Sh 25,000.

Waziri Mkuu alisema risiti ya manunuzi inaonesha kwamba walipaswa kununua vitasa ambavyo vinafunga mara tatu (3-level) lakini alipokwenda kukagua milango kwenye mabweni, ukumbi, na bwalo alikuta ni vitasa vya kufunga mara moja ( 1-level). 

“Serikali imetoa Sh bilioni 1.4 kwa kila chuo ili kufanya ukarabati wa vyuo vya elimu kikiwemo hiki cha kwenu. Ninyi mnanunua vifaa kinyume na utaratibu wa serikali, hamvikagui, mnaweka tu vitu hafifu ambavyo havidumu, haiwezekani,” amesema.

Alipoulizwa wametumia utaratibu gani kununua vifaa hivyo, Mkuu wa chuo hicho, Hamisi Njau alisema walikuwa wakitumia kamati ya manunuzi ambayo mwenyekiti wake alikuwa ni Makamu Mkuu wa chuo na katibu wake ambaye ni ofisa manunuzi.

Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho baada ya kufanya ukaguzi huo, Waziri Mkuu alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

“Rais alitoa Sh bilioni 1.4 kwa vyuo vyote ili kukarabati na kuboresha hadhi ya vyuo hivyo vikiwemo vya Monduli, Patandi, Kinampanda, Mtwara, Songea, Nachingwea, Korogwe, Kasulu na Butimba. 

“Nimeingia kwenye maktaba yenu nimeona bado vitabu vilivyopo ni vya muda mrefu, lakini kwa upande wa ajira bado tunaendelea kuajiri kwa awamu. Julai mwaka huu tuliajiri walimu 4670 na sasa hivi tumepata kibali cha kuajiri walimu 16,000,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles