22 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Majaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi

PATRICIA KIMELEMETA

JAJI Kiongozi, Dk. Eliezer Feleshi, amewataka majaji na wafanyakazi wa mahakama kufanya kazi kwa weledi ili wakistaafu waweze kuheshimika katika taifa na jamii inayowazunguka.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa kuwaaga majaji watano iliyofanyika Viwanja vya Mahakama Kuu, Dar es Salaam jana.

Majaji waliostaafu ni Fredrica Mgaya na Crecencia Makuru kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Aisha Nyerere wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Rose Temba na Salima Chikoyo kutoka Kituo cha Usuluhishi.

Jaji Feleshi alisema mahakama ni chombo muhimu cha kusimamia haki na maadili na wakifanya kazi zao kwa weledi kutawasaidia kulinda Katiba ya nchi na kusimamia sheria ambayo ndiyo mwongozo wao.

Alisema kwa wale watakaobainika kwenda kinyume na sheria, watachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.

“Majaji na wafanyakazi wa mahakama wamepewa vitambulisho maalumu ambavyo vina majina yao ili waweze kutambulika kwa jamii, ikiwa watakwenda kinyume na miiko ya kazi, maadili au kuvunja sheria watachukuliwa hatua,” alisema Jaji Feleshi.

Aliwataka wananchi wawe wanaangalia kitambulisho cha kila mtumishi pale wanapohitaji huduma za mahakama na ikiwa watakwenda kinyume wawataje kwa majina ili wachukuliwe hatua.

Alisema mahakama itaendelea kujiimarisha katika kazi zake na kuwatumia majaji waliostaafu kwa ajili ya kuwashauri, kufanya utafiti au shughuli nyingine za kimahakama pale watakapohitajika ili kuboresha majukumu ya kimahakama.

“Mahakama imekuwa na utaratibu wa kuwatumia majaji wastaafu katika shughuli mbalimbali za kimahakama ikiwamo kufanya utafiti, ushauri au kutoa maoni yao ya namna gani tufanye ili kuboresha shughuli za mahakama nchini.

“Kuna baadhi ya majaji wastaafu tuliweza kuwatumia kwenye mafunzo ya majaji wapya katika Chuo cha Mahakama cha Lushoto hivyo basi ni watu muhimu katika shughuli zetu, hatuwezi kuwaacha,” alisema.

Alisema hadi sasa majaji wastaafu wamefika 70 huku waliobaki ni 70 jambo linaloonyesha Serikali imeweza kuongeza idadi yao ili waweze kuwatumikia wananchi kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, alisema ni faraja kuona majaji wote waliostaafu utumishi wa mahakama ni wanawake na wameweza kufanya shughuli zao kwa weledi na uadilifu kulingana na shuhuda mbalimbali zilizosomwa katika hafla hiyo.

Alisema anatamani kuona majaji wanawake wanapewa kipaumbele kwenye nafasi za juu za uongozi ili kuleta chachu kwa wengine.

“Sitashangaa miaka ijayo nikiona kuna uteuzi wa Jaji Mkuu mwanamke kutokana na weledi na uadilifu ulioonyeshwa na majaji wanawake katika kutekeleza majukumu yao,” alisema Fatma.

Pia alisema hadi wanastaafu, majaji hao kwa pamoja wametoa hukumu zaidi ya 200 katika kesi mbalimbali walizozisikiliza.

Kwa upande wao, majaji hao walisema hakuna kitu kigumu wakati wa majukumu yao kama kuandika hukumu.

“Hakuna kitu kigumu kama kuandika hukumu, kwa sababu unaangalia aina ya kosa halafu jamii inakuzunguka pia, ilifika wakati nilikuwa silali kwa ajili ya kuhakikisha namaliza majukumu yangu mapema ikiwamo ya kuandika hukumu ili niweze kumaliza kesi,” alisema Temba.

Alisema jamii inapaswa kutambua kuwa kazi ya kuwa hakimu si ndogo, tena inahitaji ujasiri ili ukamilishe salama kwa sababu unatumia muda mwingi kuandika hukumu ili uweze kutoa uamuzi sahihi.

Hata hivyo, alisema alifanya kazi kwa weledi na uadilifu hadi imefika wakati wake ameweza kustaafu kwa heshima.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

 1. Naamini Watanzania wengi watakubaliana na mimi kwamba ni vigumu sana kwa watu masikini kupata haki yao wanayostahili kulingana na mfumo wa kimahakama uliopo. Maskini hana uwezo wa kumlipa wakili kwa sababu gharama zao ni kubwa sana. Tena, mfumo unaofanya mawakili wasiende kuwakilisha watuhumiwa kwenye mahakama za mwanzo unawapa mahakimu wa mahakama hizo fursa ya kutoa upendeleo usio wa haki kufaidisha matajiri walio tayari kutoa rushwa. Baya zaidi ni kwamba kuna baadhi ya waendesha mashtaka (japo ni wachache) wanakula njama na mahakimu wanapokea rushwa (na kugawana na hao mahakimu wala rushwa) ili upande mmoja kwenye hiyo kesi ugandamizwe.

  Sote tuliona juzi namna Mheshimiwa Rais alichukua hatua stahiki na kuhakikisha kwamba mtu aliyekuwa amebambikizwa kesi ya mauaji ameachiwa huru. Hili la kubambikizwa kesi mbaya lipo sana, na kuna idadi kubwa tu ya mahabusu ambao wamebambikizwa kesi kwa namna hiyo.

  MAPENDEKEZO YANGU:-
  Namwomba sana Jaji Mkuu (CJ) aunde kikosi maalum (kikiwa hakina polisi ndani yake), ambacho kitakuwa na majaji wastaafu wanaojulikana kwa weledi wao pamoja na viongozi wa dini na wa kijamii. Kazi ya kikosi kazi hiki iwe ni kupitia malalamiko yote ya wanyonge wanaolalamika kuonewa kwa kubambikizwa kesi au kuendeshewa kesi kwa namna ambayo inamnyima mshatakiwa nafasi ya kupewa haki.

  Bila haki hakuna amani. Tunapoona wananchi wanajichukulia sheria mkononi (kwa kuua watuhumiwa bila kuwaacha vyombo vya sheria viwashughulikie) haya ni matokeo ya watu KUKOSA IMANI NA MFUMO WA UTOAJI HAKI ULIOPO.

  Nashukuru kwa kupata fursa ya kutoa haya mawazo yangu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,504FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles