26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Majaji tekelezeni agizo la Jaji Mkuu

NI nadra kumsikia Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma akitoa maelekezo mazito kwa wasaidizi wake.

Amekuwa makini tofauti na watangulizi wake kadhaa. Lakini juzi alitoa maelekezo mazito kwa majaji wapya 12 walioteuliwa hivi karibuni.

Akionekana kutofurahia kitendo cha majaji wake kupewa maelekezo au amri kutoka kwa watu fulani, Jaji Juma amepiga marufuku wataalamu hawa wa sheria kupokea amri au maelekezo ya namna yoyote wakati wa kuendesha kesi zao.

Si kuendesha mashauri tu, hata wakati wa kutoa uamuzi ambao kwa namna moja au nyingine, unaweza kuonekana unampendelea mtu fulani na kumwacha mhusika akilalamika.

Tunakubaliana na Jaji Mkuu kwamba wakati wa majaji kutekeleza majukumu yao, lazima watakumbana na majaribu mengi.

Moja ya majaribu haya huwa ni maelekezo kutoka kwa mtu au kiongozi fulani ambaye ana masilahi fulani ili kutimiza lengo lake.

Siku zote jaji ambaye anapewa maelekezo na mamlaka nyingine hupoteza umakini na kushindwa kutoa haki kulingana na suala lililoko mbele yake.

Jaribu jingine ambalo tunaamini wanakumbana nalo, ni rushwa. Hapa ndipo huwa na mtihani mkubwa, lakini tukiamini majaji hawa wamepikwa na wataweza kuviepuka vikombe hivi ambavyo havina tija kwa taifa na Watanzania kwa ujumla.

nyingine watamalizia mafunzo Chuo cha Mafunzo Lushoto.

Tunaamini jaji yeyote anayepokea maelekezo hupoteza uhuru wa kuamua jambo kisheria, badala yake huamua kwa utashi wake tu, jambo ambalo halikubaliki.

Tunaamini siku zote majaji hawa wanapaswa kusoma na kuzielewa vizuri kanuni zao zinazowapa mwongozo wa uendeshaji kesi.

Kauli ya Jaji Mkuu Juma, hakika ikiishi kwenye vichwa vya majaji wetu litakuwa jambo jema na heri katika utendaji kazi wa kila siku.

Maneno haya yanapaswa kubaki kwenye viapo vya majaji hawa ambao wameviapa ili kuutumikia umma wa Watanzania. Viapo ndiyo msaafu wao mkuu ambao utawafanya waepuke kuingia kwenye majaribu.

Ni wazi kila mmoja wao atasoma kanuni  ambazo zinampa mwongozo kwa sababu ofisa wa mahakama Tanzania analindwa na misingi ya usawa, haki na maadili katika kazi zake na si nje ya hapo.

Kwa mfano, kanuni ya kwanza inamtaka kila mmoja kujikinga kuingiliwa kazi, hata kutoka kwa ndugu zake, marafiki na hata wenzake. Huu ni msaafu uliokamilika hatutegemei kusikia au kuona mambo mabaya yakifanyika.

Ni ukweli usiopingika kwamba hata ngazi ya familia, zipo zenye nguvu ambazo zinaweza kuwa na ushawishi mkubwa wa kuharibu kazi nzuri inayofanywa na majaji.

Zipo familia ambazo zinaweza kutoa mwongozo wa namna ya kufanya kazi za majaji, jambo ambalo tunasema halipaswi kupewa nafasi.

Alisema kanuni hizi zinazohusu uhuru wa kufanya kazi zinaweza wakati mwingine zikasababisha kujitoa kwenye shauri lililopo mbele yako ili ionekane uko huru.

Sisi MTANZANIA, tunasema majaji tekelezeni agizo la Jaji Mkuu ili kufikia malengo mliyojiwekea.

Itakuwa aibu kubwa kusikia jaji katembea nje ya maelekezo haya ambayo tunaamini yamelenga kujenga mhimili wa mahakama ulio imara katika utoaji wa haki. Watanzania wengi wana imani kubwa na mhimili huu. Tunawaasa hata viongozi wenye tabia ya kuingilia mhimili waache na wakae kando kabisa, waache masuala ya kisheria yaendeshwe kisheria tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles