Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM
HATIMAYE mwili wa Ernest Materego uliokuwa ukigombewa kuzikwa, utazikwa kesho katika makaburi ya Airwing, Ukonga Jeshini, Dar es Salaam.
Edwin Materego ambaye ni mtoto wa marehemu, aliliambia MTANZANIA jana kuwa mwili huo uliwasili jana kutoka Bunda.
“Tulisafirisha salama mwili kutoka Bunda hadi Dar es Salaam jana (juzi), sasa hivi tumeuhifadhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, tumepanga kwenda kuupumzisha mwili wa baba yetu mpendwa kesho katika makaburi ya Airwing na tayari tumepatiwa kibali,” alisema.
Materego alifariki dunia Novemba 19, mwaka huu na maiti yake kugombewa na watoto, mke na ndugu wa marehemu kuhusu wapi azikwe.
Wakati watoto wa marehemu walitaka kuuzika mwili wa baba yao Dar es Salaam, ndugu zake wakiongozwa na mdogo wake, Gonche Materego ambaye alikuwa akimuuguza, walitaka kwenda kuzika Bunda, mkoani Mara na tayari walikuwa wameshausafirisha.
Kutokana na mvutano huo, watoto wa marehemu Joyce, Edwin, Rita, Irene na mama yao mzazi, Dinah Willige, walipinga mahakamani wakiomba amri mwili urejeshwe Dar es Salaam wakidai ndiko baba yao aliwaambia akifariki azikwe.
Wadaiwa akiwamo mdogo wa marehemu, Gonche, mke mdogo wa marehemu, Mwajuma Hassan (39), rafiki wa marehemu Thobias Mwita (66) na majirani, walitaka mwili huo uzikwe Bunda wakidai kuwa alitaka kuzikwa kwao.
Novemba 24, mwaka huu, mahakama iliamua mwili huo wapewe watoto wa marehemu na si ndugu zake.