30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maisha yaanza kurudi upya Ulaya

ROME, ITALIA

MAMILIONI  ya watu barani Ulaya wanaanza kurudi kwenye maisha ya kawaida, baada ya wiki kadhaa za kujifungia ndani kwa hofu ya maambukizo ya virusi vya korona lakini wanakaribishwa na dunia ambayo si kama walivyoiwacha.

Anga la rangi ya bluu linawakaribisha wakazi wa Mji Mkuu wa Italia, Rome, katika dunia ambayo kamwe haitakuwa tena ile waliyoiwacha wiki kadhaa nyuma wakati walipolazimika kujifungia ndani kwa hofu za maambukizo ya virusi vya Corona. Kuna mengi yaliyobadilika na ambayo huenda yasirejee tena kwenye hali ya zamani.

Italia, taifa la pili baada ya Marekani kwa kuwa na vifo vingi vya wagonjwa wa Covid-19, limeanza rasmi shughuli za uzalishaji mali jana, Jumatatu Mei 4 kwa kufungua viwanda na maeneo ya ujenzi.

Migahawa nayo imefunguliwa, lakini kwa huduma za kuchukua tu chakula, huku baa na maeneo mengine ya starehe yakiendelea kufungwa.

Watu wanashauriwa kuepuka kutumia usafiri wa umma, na wachache wanaoutumia, wanalazimika kuvaa barakoa.

Uchumi wa Italia, ambao ni wa tatu kwa ukubwa katika Ukanda wa Euro, unatazamiwa kusinyaa katika kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu mfadhaiko wa Kiuchumi wa Kilimwengu wa miaka ya 1930. 

Kwa Marekani, taifa linaloongoza kwa maambukizo na vifo, inuko la kiuchumi lilikuwa liwe alama kuu ya mafanikio ya Donald Trump kwenye kampeni yake ya kuomba kuchaguliwa tena kuwa rais kwenye uchaguzi wa Novemba.

Lakini wiki kadhaa za zuio la shughuli za maisha limepelekea Wamarekani milioni 30 kupoteza ajira zao, na sasa kiwango cha uungwaji mkono kwa Trump kimeshuka. 

Mwenyewe Trump aliongeza mashambulizi yake dhidi ya China, akiituhumu kuwa chanzo cha kirusi ambacho anasema kilianzia kwenye maabara moja mjini Wuhan.

Kauli hiyo sasa inaungwa mkono na waziri wake wa masuala ya kigeni, Mike Pompeo, ambaye alisema ana ushahidi wa kutosha kuwa virusi vya corona ni zao la maabara za Kichina.

“Nadhani dunia nzima inaweza kuona sasa, na kumbuka, China ina historia ya kuuambukiza ulimwengu na kuendesha maabara zilizo chini ya viwango,” alisema Pompeo siku ya Jumapili bila kutaja hasa kilipo chanzo cha ushahidi wake.

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Marekani alisema kuwa bado wachambuzi wanachambua taarifa walizokusanya kujuwa asili hasa ya virusi hivyo. China, kwa upande wake, inakanusha madai hayo.

Hadi sasa wanasayansi wengi wanakubaliana kuwa ugonjwa wa Covid-19 ulitokana na jamii ya wanyama kwenda kwa wanadamu kwa utaratibu wa kawaida wa kimaumbile.

Kurejea kwa kauli hizi dhidi ya China kutoka Serikali ya Marekani kumeyatikisa masoko ya hisa, huku wawekezaji wakiwa na wasiwasi endapo zinaweza kuishia kwenye vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo makubwa duniani.

Soko kuu la hisa la Hong Kong limeshuka kwa asilimia nne, huku mengine barani Asia yakipoteza asimilia mbili na ya Ulaya yakianza Jumatatu hii kwenye mstari mwekundu.

Kiasi cha watu 248,000 wamepoteza maisha yao tangu virusi vya corona kuibuka nchini China mwishoni mwa mwaka uliopita na haraka sana kikaweza kusambaa kwenye mataifa mengine na kuwaambukiza watu wapatao milioni tatu na nusu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles