24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maisha ya Mkapa kwa waliomfahamu vyema

 ANDREW MSECHU

BAADA ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kufariki dunia Julai 23 saa 3:30 usiku jijini Dar es Salaam na kuzikwa Julai 29 saa tisa alasiri kijijini kwake Lupaso wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara, wengi wameeleza walivyomfahamu na hapa wengine zaidi wanazungumza walivyomjua kiongozi huyo.

ALIYESOMA NAYE KUANZIA DARASA LA TANO

Balozi John Kambona, ambaye alisoma na Rais mstaafu Benjamin Mkapa kuanzia shule ya kati hadi Chuo Kikuu kisha kupangiwa kazi pamoja mkoani Dodoma.

Alisema Mkapa alikuwa Ofisa Tawa wa wilaya nay eye akiwa katika idara ya kilimo.

Balozi Kambona alisema alimfahamu Mkapa tangu mwaka 1949 walipokutana katika Shule ya Kati Ndanda ambapo waliingia pamoja darasa la tano wakati huo, kisha kuanza safari iliyowafikisha mbali.

“Tulisoma pamoja pale Ndanda ila yeye alitoka muda mfupi kwenda Kigonsera na baadaye alirudi Ndanda. Halafu tulipofanya mtihani wa darasa la 10 mwaka 1954 tukatoka Ndanda tukaenda Pugu sekondari ambapo tulikaa miaka miwili na tukafaulu mtihani wa Cambridge tukaenda Makerere.

“Tulikaa wote kule Makerere tukiwa wanafunzi kwenye chuo hicho kwa miaka mitano, yeye akichukua BA in English (Shahada ya Lugha ya Kiingereza) na mimi nilichukua BACC in Botany (shahada ya mambo ya mimea).

“Tulipomaliza tulirejea nchini, tukaanza kazi mwaka 1962 yeye akiwa DEO (Ofisa Mtendaji Wialaya) posti yake ya kwanza ilikuwa Dodoma na mimi nilipangiwa kuwa ofisa kilimo nikapelekwa pia Dodoma,” alisema.

Balozi Kambona alisema kutokana na mtiririko huo waliendeela kuwa karibu na Mkapa na uhusiano wao ulizidi kukua nyakati zote baada ya hapo hadi umauti ulipomkuta, wakiwa bado ni marafiki wa karibu sana.

Balozi huyo alisema anachokumbuka kuhusu Mkapa tangu alipokutana naye ni kwamba alikuwa kijana makini sana tangu alipokuwa shule.

Alisema Mkapa alikuwa akipatia sana hesabu kwa kuwa alikuwa makini na wenzake walikuwa wanakwepa hesabu na kukimbilia masomo mengine kwa kuwa hesabu ziliwapa shida kidogo, ila kwa Mkapa, alipenda hesabu.

Alisema japokuwa baadaye Mkapa aliamua kuchukua masomo ya lugha ya Kiingereza, lakini alipokuwa shule alipenda na aliweza vizuri somo la hesabu, hivyo alikuwa mtu makini ambaye baadaye, ujuzi wake wa lugha ya Kiingereza ulimsaidia sana.

Kambona alisema anapoangalia ujana wa Mkapa, vijana wa sasa namna sahihi ya kumuenzi ni kwa kuacha tamaa, maana kio alianza katika ngazi ya chini kabisa na kwamba waswahili wanasema hata mbuyu ulianza kama mchicha.

“Ila vijana wengi, tangu zama hizo wana tamaa, anataka aanze kazi leo siku ya pili aonekane ana motokaa, mambo ambayo kwa hali ya kawaida si rahisi hivyo wafanye kazi kwa bidii na kwa utaratibu ili waendelee taratibu kutokana na mazingira na nyakati,” alisema.

PROFESA MAHALU ALIYEOKOLEWA NA JELA 

Kwa upande wake Profesa Costa Mahalu alisema atamkumbuka Mkapa kipekee kwa sababu alimkomboa na gereza kwa kuwa bila ushahidi wake, angeweza kufungwa.

Prof. Mahalu alitoa kauli hiyo akiwa kijijini Lupaso baada ya maziko ya Mkapa, akisema kesi ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma wakati akiwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mkapa aliamua kwenda mwenyewe mahakamani kutoa ushahidi akimtetea Mahalu. 

“Mkapa alinikomboa na gereza, maana bila ushahidi wake ningeweza kufungwa, licha ya kwamba sikuwa na kosa. Nilipookoka katika kesi ile nilimshukuru na nilikwenda kanisani kumshukuru Mungu,” alisema.

Prof. Mahalu alisema Mkapa atakumbukwa hasa kwa kuwa Serikali ya awamu tatu iliweka misingi imara katika kila nyanja.

Alisema alikutana na Mkapa alipoingia wizarani wakati wa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Alisema anakumbuka Mkapa akiwa Waziri wa Elimu na Teknolojia, alivyobadili sera ya eilimu ili kuruhusu watoto wengi wa masikini kupata elimu ya juu. 

“Alipendekeza tuangalie namna ambayo watoto wa wasio na uwzo wanaweza kusaidiwa kwa kuchangia gharama za elimu ya juu, tukaanzisha sera ya elimu ya juu.

“Pia alikuwa na wazo kwamba kila mwaka kuna wanafunzi wengi ambao wanafaulu na wanastahili kuchaguliwa kwenda kupata elimu ya juu wakati tulikuwa na vyuo vikuu viwili tu, kwa hiyo akasema kuna wengi ambao hawataweza kupata udahili kama tukiwa na vyuo viwili, hivyo kukawa na ulazima wa kuangalia uwezekano wa kuanzisha vyuo vikuu binafsi.

“Kwa hiyo yeye ni muasisi wa vyuo vikuu binafsi hapa nchini na wakati tukianzisha vyuo hivyo alikuja na pendekezo kwamba tuwe na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi ili tuweze kuwasaidia wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo, kwa hiyo hilo nalo likakubaliaka, tukaanzisha vyuo vikuu binafsi na bodi ya mikopo,” alisema.

Alisema pia Mkapa atakumbukwa kama waziri na rais ambaye alikuwa ametilia maanani suala la uendelezaji wa elimu ya juu kwa wote kwa kuwa aliondoa wasiwasi kwamba unapowapa elimu wachache unajenga tabaka.

Prof. Mahalu alisema mkusanyiko wa watu waliofika kumzika Mkapa unamaanisha kwamba tunahitaji kuwa watu wema, kuwa wawazi na kuwa watu wenye upendo kwa jirani

Alisema kwake yeye kama mkristo anaamini katika upendo wa Mungu na kuishi katika upendo wa kristo kwa kuwa kama asingeishi upendo wa kristo kusingekuwa na kusanyiko kubwa lililojitokeza kumhifadhi kijijini kwake Lupaso.

Alisema kabla ya kufariki Mkapa alizungumza naye akimtaka wakutane ili waangalie namna ya kuboresha seneti za vyuo vikuu na kuangalia jinsi ya kuondoa ubaguzi unaoonekana kuwepo kati ya vyuo binafsi na vya Serikali.

Alisema alikuwa na ratiba ya kuonana naye Julai 30 lakini kwa bahati mbaya suala hilo halikutimia kwasababu ya umauti uliomfika na kuzukwa Julai 29 siku moja kabla ya waliyopanga kuonana kufika.

Alisema Mkapa anastahili kuenziwa kama baba wa taifa kwa upande wa kutanua uchumi zaidi ambao utakuwa wa haki na kwa kuwa amesimamia kutokomeza rushwa na kuboresha ulipaji kodi. 

MASILINGI KAZI NA UMRI MDOGO 

Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi, alisema awamu ya tatu kwake huwa ni kumbukumbu kutokana na kupata nafasi ya kuwakiongozi akiwa na umri mdogo.

Alisema uaminifu huo ulinimpa nafasi ya kuyaishi yale aliyokuwa akielekezwa hali ambayo ilimfanya aendelee kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika Nyanja mbalimbali. 

“Niliaminiwa na Rais wa awamu ya tatu hayati Benjamin Mkapa nikapewa uwaziri wa utawala bora nikiwa kijana mdogo, kwa kweli kwangu niliona heshima kubwa nilitekeleza majukumu yangu kama nilivyoagizwa.

“Leo ni siku ya majonzi kwangu ndio maana hata kuongea nashindwa tangu nirudi nimekosa la kuongea, lakini kupitia yeye Rais John Magufuli aliniona nikapewa majukumu mazito ya kuwakilisha nchi.

“Wakati wa awamu yake alitufundisha kazi na upendo, hata umtumie ujumbe alikuwa anaujibu, nasikitika kwakuwa ameondoka akiwa hajajibu ujumbe niliomtumia mara ya mwisho,” alisema Masilingi.

 SUMAYE WAZIRI MKUU MIAKA 10

Kwa pande wake Fredrick Sumaye, akieleza namna anavyomkumbuka Mkapa, alisema ana mengi ya kumuelezea, ambayo yanahitaji muda wa kutosha.

Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 ya uongozi wa Mkapa, alisema yeye kuwa Waziri Mkuu kwa miaka yote 10 ni ishara kwamba ni mtu ambaye anaamini kuwa alimuamini sana ndiyo maana akamteua kwa vipindi vyote viwili.

“Lakini nilipofanya naye kazi, nilibaini kuwa ni mtu ambaye ana msimamo mkali na jambo lake akishaliamua anataka lifanikiwe, lakini ni mtu ambaye unafurahia kufanya naye kazi kwa sababu anakueleza kile ambacho angependa kifanyike.

“Pili alikuwa ni mtu ambaye mkishakubaliana hana muda tena wa kukufuata fuata, anategemea utatekeleza majukumu yako kwa hiyo ni mtu ambaye mimi binafsi nilikuwa nafurahia kufanya naye kazi sana,” alisema.

Sumaye alisema ana mambo mengi ya kukumbuka kwa sababu ni Mkapa aliyemfikisha kwenye uwaziri mkuu na hakumuacha, aliendelea kumlea akiwa kama mwalimu wake na mafanikio mengi ya Serikali ambayo waliyafikia wakati wa uongozi wao ni mambo ambayo mtu yeyote anaweza kujivunia, kwa hiyo anamkumbuka kwa mambo mengi.

Alisema anapenda kuwaasa vijana kuwa wanatakiwa kutambua fursa zipo nyingi na kinachotakiwa ni kuzitumia fursa hizo.

 Alisema kwa uzoefu wake, tatizo kubwa la vijana nchini ni kufikiria ajira za Serikalini au za kwenye kampuni ambazo haziwezi kutosha katika nchi yoyote.

“Kwa hiyo Mkapa alikuwa ni mtu aliyejaribu kutengeneza fursa ili vijana waweze kuzitumia na kujitegemea bila kutegemea kuajiriwa, kwa hito ninawaasa vijana kwamba hebu tujitahidi, tusitegemee tu fursa za ajira.

“Kwa hiyo ninaamini tukifuata mambo ambayo alikuwa anayasema na kuyasimamia Mkapa tutafanikiwa sana,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles