Mwandishi wetu, Mbeya
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga, amesema Tanzania ina mgawanyo wa madaraka na unaofuatwa vizuri tofauti na nchi nyingine.
Akizungumza juzi alipotembelea Ofisi za Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mahiga alisema ametembea nchi mbalimbali na kujifunza kwamba Tanzania mgawanyo wa madaraka unafuatwa.
“Mgawanyo wa madaraka kwa mihimili ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama upo na unafuatwa vizuri kulinganisha na nchi nyingine ambapo hata kuonekana haionekani kabisa na kama ilikuwepo basi ilikufa,” alisema Mahiga.
Akizungumzia kazi inayofanywa Majaji ya kusikiliza mashauri ambapo kuna wakati wanalazimika kufanya kazi kwa zaidi ya saa 18 kwa siku, alisema anatambua mchango zinazowakabili.
Pamoja na pongezi hizo, aliwataka majaji hao, kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na utendaji uliotukuka.
Aliwashauri majaji kuwa na maadili ya ziada na kuufanya Mhimili wa Mahakama kutekeleza majukumu kwa viwango vya juu.
Mahiga alisema kupitia kuongezeka kwa watu na kukua kwa Sayansi na Teknolojia, nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha watu kubuni njia nyingi za uhalifu.
Alisema changamoto hizo zinasababisha kuwa na uhaba wa majaji kitendo kinachowalazimu kuwa na makadirio ya kusikiliza mashauri mengi zaidi tofauti na mipango ya kitaasisi na kila mmoja kulazimika kufanya kazi kwa muda mrefu.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Dk John Utamwa, alisema mikakati ambayo imekuwa ikitumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya katika kuhakikisha mashauri yanaamuliwa kwa wakati ni uwepo wa miongozo ya utoaji huduma.
Akitoa mfano wa miongozo hiyo alisema ni pamoja na kuhakikisha kabla ya siku 21 nakala za hukumu zinatakiwa kuwa tayari lakini Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya nakala za hukumu hutolewa ndani ya siku ambayo hukumu hutolewa.
Mahiga yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mbeya, ambapo ameambatana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga ambao wanakagua magereza na kutambua changamoto zinazowakabili wafungwa na mahabusu.