24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAHANGA KUKAMATWA MUDA WOWOTE

Na KULWA MZEE-
DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetoa hati nyingine kwa Polisi Mkoa wa Ilala ikielekeza wamkamate na kumfikisha mahakamani hapo Jumatatu (Machi 13, mwaka huu), aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga.

Hati hiyo imetolewa juzi na Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu, Ruth Masambu, baada ya kushindwa kutekelezwa amri ya awali iliyotolewa  Machi 7, mwaka huu ya kukamatwa kwake na kufikishwa mahakamani hapo Machi 9, mwaka huu.

Juzi mahakama hiyo ilimkabidhi hati hiyo Mwanaharakati wa Haki za Binadamu katika masuala ya elimu nchini, Kainerugaba Msemakweli, ambaye ni mlalamikaji katika shauri hilo alilomfungulia Mahanga ambaye
aliamriwa kumlipa mwanaharakati huyo kila mwezi sehemu ya zaidi ya Sh milioni 11 za kesi ya madai aliyomshinda.

Mlalamikaji huyo alikabidhiwa hati hiyo na kutakiwa kumkabidhi Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni mwenyewe ili aweze kutekeleza
hilo. Jana Kamanda wa Polisi huyo, Hamduni alikiri kupokea hati hiyo ambapo alisema anatakiwa kumfikisha Mahanga mahakamani Jumatatu saa 2.30 asubuhi.

Kamanda Hamduni alisema hati hiyo alikabidhiwa jana kati ya saa nane na tisa alasiri na kwamba bado hawajamkamata Mahanga, hivyo wanaendelea kumtafuta.

Mahanga anatakiwa kumlipa mwanaharakati huyo kutokana na kesi aliyokuwa amefunguliwa baada ya kesi yake ya madai ya kashfa dhidi ya mwanaharakati huyo kufutwa mahakamani.

Awali, Machi 2, mwaka huu mahakama hiyo ilitoa amri ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani hapo Mahanga kutokana na kushindwa kufika siku hiyo bila ya taarifa.

Mahanga alitakiwa kufika mahakamani hapo ili aweze kulipa Sh milioni mbili, zikiwa ni sehemu ya deni la zaidi ya Sh milioni 11 anazodaiwa na Msemakweli ambapo hati ya kumkamata na kumfikisha mahakamani hapo, ilitolewa Machi 7, mwaka huu kwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ikimwelekeza kumkamata na kumfikisha mahakamani hapo Machi 9, isipokuwa tu kama atalipa Sh 11,097,000.

Mwaka  2009, Mahanga alifungua kesi ya madai namba 145 ya mwaka 2009 dhidi ya Msemakweli na wenzake akiwemo mwandishi wa Nipashe, Muhibu Said, kwa kile alichodai kukashifiwa kutokana na mlalamikiwa huyo kuandika kitabu alichokiita Orodha ya Mafisadi wa Elimu Tanzania
ambacho Dk. Mahanga alitajwa kuwa ni mmoja wa vigogo wenye shahada za udaktari wa falsafa za kughushi.

Wadaiwa wengine walikuwa ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Nipashe lililokuwa limechapisha habari hiyo na Kampuni ya The Guardian Ltd inayomiliki gazeti hilo ambapo alikuwa akiiomba mahakama kuwaamuru wadaiwa kumlipa Sh bilioni tatu kama fidia ya madhara aliyoyapata kutokana na habari hizo alizoziita za uongo.

Hata hivyo, shauri hilo lilifutwa mahakamani hapo Julai mosi, 2014 mbele ya Jaji Salvatory Bongole, baada ya Dk. Mahanga wala wakili wake Kennedy Mfungamtama, kutofika mahakamani mara kadhaa licha ya
kupatiwa hati ya wito kwa tarehe zilizokuwa zikipangwa.

Baada ya hapo, Msemakweli aliamua kufungua kesi ya madai dhidi ya Dk. Mahanga, akiiomba mahakama pamoja na mambo mengine kumwamuru mlalamikiwa amlipe gharama za kesi hiyo ambapo mahakama ilimwamuru
Mahanga amlipe mdai huyo Sh milioni 14 na amlipe Muhibu Sh milioni 33.

Lakini tangu Juni, 2016, Dk. Mahanga alimlipa Msemakweli Sh milioni moja tu na kuamua kutofika mahakamani, jambo ambalo lilimfanya Msemakweli kuwasilisha maombi akiomba Mahanga afungwe jela kwa kushindwa kutekeleza amri ya mahakama ya kumlipa deni hilo.

Kutokana na hilo, Desemba 2, 2015 mahakama ilimwandikia Mkuu wa Gereza la Ukonga barua ikiomba mchanganuo wa gharama za kumtunza gerezani mdaiwa
huyo, ambapo majibu yalitoka na mahakama ilimtaka Msemakweli awasilishe mahakamani Sh 300,000 kama kianzio kumgharamia mdaiwa huyo kwa mahitaji ya chakula na mengine atakapokuwa
amefungwa gerezani.

Msemakweli aliwasilisha fedha hizo ambapo Mahanga alifika mahakamani
hapo na kuomba alipe ambapo alikubaliwa awe anamlipa Sh milioni 2.8 kila mwezi. Hata hivyo, Mahanga alilipa mwezi mmoja Sh milioni moja na hakuendelea kulipa tena wala kufika mahakamani.

Januari 23, mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa amri kwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Ilala ikimwagiza kumkamata na kumfisha mahakamani Mahanga Januari 31, ili ajieleze kwanini asifungwe jela kwa kuipuuza mahakama.

Januari 30, mwaka huu, Mahanga alitiwa mbaroni na Januari 31 alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi wa polisi, ambapo Msemakweli alieleza tayari ameshawasilisha mahakamani hapo Sh 300,000
za kumhudumia mdaiwa huyo gerezani wakati akitumikia kifungo chake kama mfungwa wa madai.

Mahakama kwa huruma zake ilimpa nafasi kwanza Mahanga aseme namna atakavyolipa fedha hizo kuanzia siku hiyo na aliomba alipe Sh 500,000 na aruhusiwe kuwa analipa kiasi hicho kila mwezi hadi deni
hilo litakapomalizika. Mdai huyo aligoma na kusisitiza mdaiwa apelekwe jela ambapo baadaye alidai atakuwa analipa Sh milioni moja ambayo mdai huyo aliigomea na hatimaye ikakubalika awe analipa Sh milioni mbili.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles