Na BALINAGWE MWAMBUNGU,
MAHAKAMA Kuu ya Kenya imefanya uamuzi ambao watu wengi hapa nchini, na pengine kote barani Afrika, wanatamani ungeleta faraja kwao, ili kuondokana na chaguzi ‘feki’ zinazotumiwa na watawala kuendeleza tawala zao.
Laiti kama mahakama kuu za nchi nyingine, ikiwamo Tanzania, zingekuwa na ujasiri kama huo, ni wazi kuwa demokrasia ingekomaa.
Gazeti dada la RAI limeandika habari za uchambuzi: “Mahakama zafungua milango ya haki kwa wapinzani’ (Rai Juni 28-Julai 5, 2017). Katika uchambuzi huo, Mwandishi Hilal K Sued amechambua uamuzi wa kihistoria uliofanywa na mahakama mbili tofauti—Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ambayo iliamua kuwa spika wa Bunge la nchi hiyo, anao uwezo wa kuamua upigaji kura uwe wa namna gani, wa wazi au wa siri—endapo kuna hoja ya kutokuwa na imani na rais wa nchi hiyo. Ni dhahiri kuwa, uamuzi huu unafungua milango na kupanua demokrasia ndani ya Bunge la Afrika Kusini.
Tulishuhudia jinsi jambo hili lilivyosababisha mvutano mkali katika Bunge la Katiba mwaka 2015—wale wa chama tawala waling’angania utaratibu wa mayowe wa “Ndiyooo!” hata kama dhamiri zao ziliwasuta. Kura ya siri inabaki kuwa siri ya aliyepiga kura na kutokana na hali halisi ilivyokuwa wakati ule, upepo mbaya ulikuwa unavuma kwa upande wao. Spika wa Bunge lile akaamua ipigwe kura ya wazi, kwa njia hiyo wangeweza kubainika ni kina nani walikuwa wanapinga chama chao.
Bunge la Afrika Kusini, kutokana na uamuzi wa Spika, litakuwa huru zaidi kufanya uamuzi wa kumshitaki Rais au la, hata angali akiwa madarakani.
Rais Jacob Zuma amekuwa na wakati mgumu katika utawala wake kutokana na kashfa mbalimbali—zikiwamo rushwa, ufujaji wa fedha za umma na kuzitumia kujenga kasri yake binafsi na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuipa upendeleo wa mikataba na familia ya wahamiaji ya Gupta.
Uamuzi mwingine wa kupigiwa debe, ni ule wa Mahakama Kuu ya Kenya wa kuruhusu wapinzani kufanya maandamano kila Jumatatu, ili kushinikiza uundwaji upya wa Tume ya Uchaguzi.
Kwa mwaka jana (2016) ilikuwa kila Jumatatu katika baadhi ya miji nchini humo, kulikuwa na vurugu kubwa ambazo zilisababisha shughuli zote za kibiashara, usafiri na hata masomo shuleni kusimama—maandamano hayo yalifanikiwa baada ya Mahama Kuu ya nchi hiyo kukataa kupiga marufuku maandamano hayo, ambayo yalikuwa yanaratibiwa chini ya mwavuli wa CORD (Coalition for Reforms and Democracy), yakiongozwa na Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetengula.
Pili, maandamano hayo yalikuwa na lengo la kushinikiza kuondolewa kwa makamishna wa zamani wa Tume Huru ya Ukaguzi na Mipaka (IEBC).
Hata hivyo, Mahakana hiyo hivi karibuni imefanya uamuzi mwingine ambao utaleta mabadiliko makubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya, utakaofanyika Agosti 8, mwaka huu.
Mahakama imeupa faraja sana upande wa upinzani—kwamba matokeo ya kura, kila msimamizi atatangaza matokeo yote—ya Wabunge na Rais—yatatangazwa moja kwa moja na wasimamizi wa uchaguzi katika kila kituo na kwamba sasa hapatakuwa na haja ya kusubiri tangazo la IEBC, kuhusu nani atakuwa ameshinda, hasa kwenye kiti cha urais.
Uamuzi huu ni wa busara sana, ikikumbukwa kwamba, ucheleweshaji wa matokeo ya kiti cha rais ulisababisha mfarakano mkubwa nchini humo mwaka 2007/8, ambayo yalisababisha zaidi ya watu 600,000 kukimbia makazi yao, achilia mbali waliopoteza maisha na mali zao.
Kadiri siku ya uchaguzi inapokaribia hali inazidi kuwa tete nchini humo, huku wapinzani wakidai kwamba taratibu za maandalizi zinakiukwa kwa makusudi, ili kuupa ushindi Muungano wa Jubilee Party, unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
Wapinzania kwa mara nyingine wakaenda Mahakamani na kuomba kuwa kura zitangazwe moja kwa moja na wasimamizi wa vituo (returning officers), kwa kuwa walikwisha baini kulikuwa na mipango ya kuiba kura. Kabla ya Tume mpya kuteuliwa, iligundulika kuwa majina ya wapiga kura waliofariki, waliosajiliwa mara mbili, na wengine wenye umri mdogo hayakufutwa, hata baada ya makamishina wapya kuteuliwa.
Uamuzi wa Mahakama kuwa kura zitangazwe moja kwa moja kutoka kila kituo, umezua hofu kwa watawala, kwamba huenda wakashindwa katika uchaguzi ujao. Hii itaondoa shauku (anxiety) na mikusanyiko ya kusubiri matokeo.
Mahakama Kuu ya Kenya, ambayo imekuwa ikiamua kesi nyingi zinazotokana na chaguzi tata tangu mfumo wa vyama vingi urejewe, imeonyesha mfano wa kuigwa. Tunatamani hata Mahakama Kuu ya Tanzania ingeiga mfano huu mzuri. Makatazo ya kutofanya mikutano ya siasa, yanawanyima wananchi uhuru wao wa kikatiba. Kuwaamrisha wananchi kwamba mwanasiasa akitaka kufanya mkutano—hata wa ndani, sharti aombe kibali cha Jeshi la Polisi—jambo ambalo Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, imetamka kuwa ni kinyume cha sheria.
Katika majumuisho yake, Jaji Mlacha alinukuliwa akisema wakati anawaachia washitakiwa wawili—wanachama wa Chadema, Suleiman Mathew na Ismail Kupilila, kwamba Jeshi la Polisi kisheria, halina mamlaka ya kutoa vibali kwa ajili ya maandamano au mikutano ya hadhara.
Wenzetu Kenya wametutangulia!