31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Mahakama yawaonya Prof. Lipumba, Mdee

HALIMANA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaonya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na wenzake kwa kuchelewa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa kutohudhuria mahakamani.
Washtakiwa hao walionywa kwa nyakati tofauti jana wakati kesi zao zilipokwama kuendelea kusikilizwa kwa sababu yao.
Kesi inayomkabili Profesa Lipumba na wenzake 31 ilitakiwa kuendelea kusikilizwa, lakini iliahirishwa kwa sababu hakimu anayeisikiliza, Cyprian Mkeha hakuwapo na washtakiwa walichelewa kufika mahakamani.
“Mahakama inatoa onyo kwa Profesa Lipumba na wenzako 31 kwa kuchelewa kufika mahakamani, utaratibu wa mahakama kesi zinaanza saa tatu kamili asubuhi, mnatakiwa kuheshimu muda sababu kila mtu anaishi mbali.
“Nimewapa onyo, kesi itaendelea Julai 10 mwaka huu washtakiwa wote mnatakiwa kuwahi,” alisema Hakimu Huruma Shahidi aliyeahirisha kesi hiyo.
Profesa Lipumba na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya maandamano bila kibali na kukaidi amri halali ya polisi iliyowataka kutawanyika Januari 27, mwaka huu.
Wakati huo huo, mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda imemuonya Mdee kwa kutohudhuria mahakamani na kwamba iwapo hatafika Julai 6, mwaka huu itatoa hati ya kumkamata.
“Kinachoendelea ni maneno yasiyo na ushahidi, mshtakiwa hayupo na wadhamini hawapo, tutenganishe siasa na mahakama, ifike wakati tuheshimu mahakamani, hakuna sababu ya kuendelea na kesi kama mshtakiwa hayupo.
“Tarehe ijayo Julai 6 awepo mahakamani ili kesi iendelee kusikilizwa, iwapo hatafika sitajali mbunge wala katibu kata, nitatoa hati ya kumkamata,” alisema Kaluyenda.
Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Benard Kongola akisaidiana na Joseph Maugo, waliomba mahakama itoe hati ya kumkamata mshtakiwa kwani sababu za kutofika mahakamani hazina msingi.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala akisaidiana na John Mallya walidai Mdee anahitaji ruhusa ya Spika wa Bunge ndiyo atoke bungeni.
Mbali na Mdee, washtakiwa wengine ni Renina Leafyagila na Sophia Fanuel.
Washtakiwa wengine, Rose Moshi, Anna Linjewile, Mwanne Kassim, Edward Julius, Martha Mtiko na Beatus Mmari waliachiwa huru.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Oktoba 4, mwaka huu, katika Mtaa wa Ufipa, uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam, isivyo halali, washtakiwa walikiuka amri halali ya Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf iliyowataka kutawanyika.
Ilidaiwa kuwa siku na mahali lilipotokea tukio la kwanza, washtakiwa walifanya mkusanyiko isivyo halali kwa lengo la kuandamana kwenda Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles