27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yamtaka Lissu, yakataa sababu wadhamini

KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema haikubaliani na sababu iliyolewa na mdhamini wa aliyekuwa  Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kwamba mshtakiwa anatafuta wadhamini hivyo hakuweza kufika mahakamani.

Lissu ameteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kugombea urais wa Tanzania na sasa anazunguka kwenye mikoa mbalimbali kutafuta watu wa kumdhamini baada ya kuchukua fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Jana Mahakama ya Kisutu ilisema sababu iliyotolewa na mdhamini wa Lissu mahakamani hapo haikubaliki kisheria na suala la mshtakiwa kugombea uwe ubunge ama udiwani haliihusu mahakama.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alisema hayo jana wakati kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu na wenzake ilipokuwa inatajwa.

Wakati kesi hiyo ikitajwa jana Lissu na mshtakiwa Ismail Mehboob hawakuwepo mahakamani lakini wadhamini walikuwepo.

Mdhamini wa Ismail, Juma Othman alidai mshtakiwa anaumwa na kutoa nyaraka za kuonyesha mgonjwa.

Mdhamini wa Lissu, Robert Katula alidai kafanya mawasiliano na Lissu jana asubuhi, akamweleza kwamba yuko mkoani anatafuta wadhamini kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.

Hakimu Simba baada kusikiliza sababu hiyo alihoji kama mdhamini anaiona inakubalika kisheria.

” Unaona sababu zako zinakubalika kisheria? Mtu kugombea ubunge au udiwani sisi haituhusu,”alisema Hakimu Simba ambapo  Katula alidai anaiachia mahakama iamue.

“Ukisema unaiachia mahakama nitakwambia ulipe dhamana japo kuwa nitakuwa nakuonea, hizo sababu zako hazikubaliki kisheria na tusiikosee sheria.

“Nenda nyumbani, tarehe ijayo tunamtaka mtuhumiwa wetu,” alisema Hakimu Simba na kuahirisha kesi hadi Septemba 14 mwaka huu.

Lissu na wenzake wanne katika kesi ya msingi wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo  kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kati ya  Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir Idrisa, Simon Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Ismail Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha Gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles