28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yamsubiri mteule wa Mwakyembe

kipandeNa Masyaga Matinyi, Dar es Salaam

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA, Mhandisi Madeni Kipande, aliyesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali zilizoainishwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, imebainika kuwa anakabiliwa na mashtaka mengine ya ubadhirifu na rushwa.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya uhakika kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kipande alipaswa kupandishwa kizimbani tangu 2010, lakini haijajulikana sababu ya kutofikishwa mahakamani hadi sasa.
Kabla ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Kipande alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani wakati huo ikiwa Wizara ya Miundombinu ambapo kwa sasa ni Wizara ya Ujenzi.
Taarifa hizo zimesema akiwa Wizara ya Miundombinu mwaka 2008, alituhumiwa kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu kwa kushirikiana na mmoja wa watumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ambaye kwa sasa jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kitaaluma.
Chamzo chetu kilisema: “Hawa walikuwa wakituhumiwa kutumia fedha za Serikali katika kutengeneza matangazo ya ujumbe wa usalama barabarani na kuyarusha katika Televisheni ya Taifa, matangazo ambayo gharama za utayarishaji zilipandishwa juu tofauti na gharama halisi na kuisababishia Serikali kuingia hasara ya mamilioni ya fedha.
“Tuhuma hizi ziliripotiwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mwaka 2008, ili ziweze kufanyiwa uchunguzi na kubaini kama watuhumiwa walihusika katika ubadhirifu huo.
“Kama ilivyo kawaida, Takukuru tulianza uchunguzi wetu ambapo watuhumiwa walihojiwa pamoja na baadhi ya mashahidi na jalada la uchunguzi lenye namba PCCB/KND/ENQ/05/2008 lilifunguliwa.
“Tulifanya kazi yetu ya uchunguzi na kuikamilisha na kama ilivyo kawaida jalada husika lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) tarehe 25/01/2010 kwa ajili ya kuombewa kibali cha mashtaka.
“Oktoba 23, mwaka 2012 jalada husika lilirudi kutoka kwa DPP likiwa na kibali cha mashtaka kwa maana kwamba Mhandisi Kipande pamoja na mwenzake walipatikana na tuhuma, hivyo kuruhusu Takukuru kuwafikisha mahakamani.
“Kitu ambacho ni cha kushangaza zaidi ni kwamba Kipande wakati anateuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, tayari alikuwa ni mtuhumiwa na anatakiwa kufikishwa mahakamani, na hakuna aliyetoa hoja kuwa mhusika ni mtuhumiwa asipewe majukumu hayo.”

KIPANDE AWA MBOGO

MTANZANIA ilipomtafuta Mhandisi Kipande kuhusu suala hilo, alijibu kwa ukali akisema: “Msinisumbue, hilo suala nalifahamu na lilishakwisha. Najua ninyi hamna lolote mnataka pesa, siwapi hata senti tano.
“Na kama mnataka nikamatwe, basi andikeni Hoseah (Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah) aje anikamate, si anajua ofisi yangu ilipo? Na sasa hivi sikubali, mkiniandika lazima niwashtaki.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Hoseah alipoulizwa kuhusu kuchelewa kupelekwa mahakamani kwa Kipande, alisema si utaratibu kuzungumzia utendaji wa ndani wa taasisi hiyo kwenye vyombo vya habari.
“Nisingependa kuzungumzia hilo suala, lakini ikumbukwe hakuna mtu aliye juu ya sheria,” alisema Dk. Hoseah.
Alipotafutwa jana kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, alisema ni vema suala hilo likazungumzwa na Takukuru wenyewe.
Jumatatu wiki hii, Waziri wa Uchukuzi, Sitta, alitangaza kumsimamisha kazi Mhandisi Kipande na kuunda timu ya uchunguzi kuchunguza tuhuma dhidi yake, kwa wiki mbili kabla ya kumkabidhi ripoti.
Katika taarifa yake, Sitta alisema tangu ameingia wizarani hapo, amekuta matatizo makubwa ya kiutendaji yanayomhusisha Mtendaji Mkuu Kipande moja kwa moja ikiwa pamoja na uhusiano mbaya kati yake na wadau na wateja wa mamlaka, kukiuka kwa makusudi kwa taratibu za manunuzi na mahusiano mabaya kati yake na wafanyakazi wa mamlaka kwa ujumla wake.
Alisema TPA ipo katika kipindi cha misukusuko mikubwa ya kiutawala jambo linaloashiria hatari ya anguko kubwa la uchumi wa nchi.
“Hatari hii itagusa kwa kiasi kikubwa nchi jirani ambazo tegemeo lake ni bandari za mamlaka. Nchi hizi hupitisha wastani wa asilimia 30 ya jumla ya shehena yote inayohudumiwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” imesema taarifa ya Waziri Sitta na kuongeza:
“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya makusanyo yote ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatokana na Kodi ya Ushuru wa Forodha (Customs and Excise Duty). Kati ya makusanyo hayo asilimia 87 yanakusanywa kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Hii inaonyesha kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina mchango mkubwa katika makusanyo ya mapato ya taifa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles