33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yajivunia kasi ya kusikiliza mashauri ya jinai

Na Mwandishi wetu – Dar es Salaam

KASI ya kusikiliza mashauri ya jinai katika mahakama za wilaya hadi rufani nchini imeongezeka ambapo kati ya Januari hadi Julai Mosi mwaka huu, mashauri 25,950 yamesikilizwa.

Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Deusdedith Kamugisha, alisema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya uendeshaji  wa mashauri kwenye kikao kazi cha robo mwaka ya pili ya mwaka wa  kimahakama kilichohusisha wadau wa Kamati ya Kitaifa ya  Haki Jinai.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na mahakama jana, ilisema Kamugisha alisema hivi sasa mahakama ina uwezo wa kusikiliza mashauri yote yanayoingia na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

 ‘‘Taarifa hii inaelezea hali ya ufunguaji na usikilizaji wa mashauri ya jinai kwa kipindi cha Januari hadi Julai Mosi 2020 kwa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, mahakama za hakimu mkazi na mahakama za wilaya nchi nzima.

Alisema kwa upande wa Mahakama ya Rufani Tanzania, mashauri ya jinai 297 yalifunguliwa na mashauri 210 yalisikilizwa ikiwa ni sawa na asilimia 70.7 ya mashauri yaliyofunguliwa katika kipindi hicho.

 Kamugisha alisema wastani wa mzigo wa mashauri katika mahakama ya Rufani ni mashauri 737 kwa jopo la majaji wa tatu.

Alisema Mahakama Kuu ya Tanzania, mashauri ya jinai 2,561 yalifunguliwa na 2,618 yalisikilizwa ikiwa ni sawa na asilimia 102.2 na kwamba wastani wa mzigo wa mashauri ni  345 kwa kila Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kamugisha alisema katika mahakama za hakimu mkazi mashauri 5,338 yalifunguliwa na 5,566 yalisikilizwa ikiwa ni sawa na asilimia 104.3 ya mashauri ya jinai yaliyofunguliwa hivyo wastani wa mzigo wa mashauri ni  198 kwa kila hakimu.

 “Mahakama za wilaya mashauri 16,169 yalifunguliwa, 17,254 yalisikilizwa ikiwa ni sawa na asilimia 97.5. Hadi kufikia Julai Mosi, 2020 wastani wa mzigo wa mashauri kwa mahakama za wilaya ni 96 kwa kila hakimu,” alisema.

Alisema  mashauri 333 yalifungiliwa katika mahakama za watoto ambapo 302 yalisikilizwa ikiwa ni sawa na asilimia 90.6.

Naye Naibu Kamishna wa Polisi Saleh Ambika, aliyewakilisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, alisema  lengo kuu la ofisi yake ni kuhakikisha upelelezi wa makosa ya jinai unafanyika na unakamilika haraka zaidi kadri iwezekanavyo.

 “Upelelezi wa makosa ya jinai una hatua mbalimbali na unahusisha taasisi mbalimbali za mfumo wa haki jinai, kuna wakati mwingine polisi wanahitaji kupata ripoti zinazotoka mamlaka nyingine kukamilisha upelelezi ili kumfikisha mtuhumiwa mahakamani kwa wakati,” alisema Ambika.

Alisema upelelezi unaohusisha sampuli za kitu fulani, Kitengo cha Upelelezi lazima kishirikiane na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakati na mwingine si rahisi kupata ripoti upesi kadri ya matarajio ya upelelezi kwasababu taasisi hiyo pia inataratibu zake za kiuchunguzi.

Ambike alisema ushirikiano wa wadau hao upo kwa kiwango cha kutosha, lengo la kamati hiyo ni kuisaidia Mahakama ya Tanzania kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani. 

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Uangalizi kwa wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje ya Magereza, Charles Nganze, alisema wafungwa 706 walitumikia adhabu mbadala ya kufanya usafi wa mazingira kwenye maeneo ya Makaburi ya Kinondoni, Mabwawa ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa) wizara na zahanati mbalimbali.

Naye Kamishna Msaidizi wa Magereza, Willington Kamuhuza, alisema jitihada zilizofanywa na wadau hao zimesaidia kupunguza msongamano wafungwa kwa asilimia 0.73.

Pia aliongeza kwamba kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika mikoa 16 mashauri mbalimbali ya watuhumiwa  yamesikilizwa kwa njia ya Mahakama Mtandao baada ya kuwezeshwa kuwa na vifaa vya Tehama kutoka Mahakama ya Tanzania.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uondoshaji wa Mashauri ya Jinai, ambaye pia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Sharmillah Sarwatt alisema lengo la kikao hicho ni kutathmini utendaji kazi na kupanga  mikakati ya kupunguza mlundikano wa mashauri  ya aina hiyo. 

Kukatika mawasiliano ya barabara kati ya

Katavi, Tabora kuwa historia – Kamlwelwe

Na Walter Mguluchuma

Katavi

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amesema barabara ya kutoka Mpanda kwenda Tabora imepatiwa mwarobaini baada ya kutengenezwa kwa daraja la Mto Koga linaloiunganisha mikoa ya Tabora na Katavi hivyo itatumika kipindi cha mwaka mzima bila kufungwa.

 Kamlwelwe aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kamsisi, Inyonga na Uzega wilayani Mlele mara baada ya kumaliza kukagua barabara inayotoka Inyonga kwenda Tabora inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema kwa kipindi kirefu barabara ya kutoka Mpanda kwenda Tabora ilikuwa ikifungwa wakati masika kufuatia  daraja linaloiunganisha mikoa hiyo kuwa linajaa maji.

 Alisema ujenzi wa daraja la Mto Koga unafanywa na Kampuni  ya China Wu Yico LTD  inayojenga barabara hiyo kuanzia  Komanga  hadi Kasinde  yenye  urefu wa kilometa 108 kwa gharama ya Sh bilioni 140.

Kamwelwe alisema mvua kubwa zilizonyesha msimu huu zimewasaidia kuongeza urefu zaidi wa daraja hilo hivyo hata mvua zikinyesha nyingi kiasi gani haitatokea tena kwa daraja hilo kujaa  maji na magari kushindwa kupita .

 Alisema wananchi wa Mkoa wa Katavi walikuwa wakisikia tu lami na sasa  Serikali imewapatia na tayari wameisha iona ikiendelea kuwekwa kwenye barabara hiyo  muhimu kwa Mkoa wa Katavi na  Tanzania kwa ujumla .

 Naye Mwandisi wa mradi huo, Tendai  Kanda, alieleza kuwa kuanzia Oktoba daraja hilo litakuwa limekamilika na magari yatakuwa yakipita.

 Alisema hadi sasa ujenzi wa barabara hiyo  kwa kiwango cha lami na ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia  60 na wanatarajia kumaliza kwa wakati .

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa  Katavi, Martin Mwakabende, alisema  mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulianza Aprili 19 mwaka 2018 na unatarajia kukamilika Aprili mwakani.

 Diwani Kata ya Inyonga, Sudi Mbogo, aliyemaliza muda wake alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutaufanya Mji wa Inyonga kutokuwa kisiwani tena wakati wa masika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles