27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAGOMA KUPOKEA KIELELEZO KESI YA WEMA

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imegoma kupokea kielelezo cha bangi inayodaiwa kukutwa nyumbani kwa mlimbwende, Wema Sepetu.

Mahakama hiyo iligoma kupokea kielelezo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati akitoa uamuzi kutokana na hoja za kupinga kupokelewa zilizowasilishwa na Wakili wa Wema, Tundu Lissu.

Awali, shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula, aliomba kutoa bangi kama kielelezo katika kesi hiyo mahakamani.

Alidai alipima msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kukutwa nyumbani kwa Wema na kugundua ni bangi.

Mulima aliomba kuitoa bahasha iliyofungwa, yenye muhuri, saini ya shahidi huyo na namba ya maabara 291 ya 2017 mahakamani hapo kwa utambuzi.

Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi hivyo bahasha hiyo iliyofungwa ilipokelewa kwa utambuzi na shahidi alidai ndani ya bahasha kulikuwa na msokoto mmoja, vipisi viwili ndani yake vina majani ya bangi na akaomba kuifungua.

Shahidi aliifungua bahasha na kuomba kutoa msokoto mmoja na vipisi viwili vya bangi mahakamani kama kielelezo cha ushahidi.

Wakili Lissu alipinga kisipokelewe kama kielelezo cha ushahidi kwa sababu ndani ya bahasha hiyo kuna vitu zaidi ya msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kuwa ni bangi.

“Mheshimiwa hakimu vipisi viwili vyenye majani ukiviangalia kwa makini ni vishungi vya sigara ambayo imetumika kwa sababu vina alama ya kuungua, kwetu vinaitwa twagooso.

“Kitu kinachoitwa msokoto wa bangi hakijulikani kimefungwafungwa tu karatasi, kuna kibiriti, karatasi nyekundu, haiwezekani vitu vilivyotolewa kwenye bahasha kuwa ndivyo vitu shahidi alivielezea, mahakama isikubali kuvipokea kama kielelezo,” alidai Lissu.

Akijibu Kakula alidai pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi halina msingi wa kisheria.

Alidai vitu vilivyokuwamo ndani ya bahasha msokoto mmoja na vipisi viwili vya bangi, hakuna kitu ambacho shahidi huyo kakisema kimekutwa hakipo na kwamba hivyo vitu vingine haviathiri kesi.

Kakula alidai shahidi hawezi kuzungumzia kila kitu vitu vya msingi vipo, hivyo aliomba vipokelewe kama kielelezo.

“Mheshimiwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi nzito ambayo ikithibitika wanaweza kwenda jela, shahidi alitakiwa kueleza kila kitu kilichomo katika bahasha,” alidai.

Baada ya mahakama kugoma kupokea kielelezo hicho, imepanga kuendelea kusikiliza ushahidi wa Jamhuri Septemba 12 na 13, mwaka huu.

Awali katika ushahidi wake, Mulima alidai kuwa Februari 8, 2017 akipokea sampuli ya mkojo wa Wema na baada ya uchunguzi iligundulika katika mkojo wake kuna chembechembe za dawa za kulevya aina ya bangi.

Wema, Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas, wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Inadaiwa Februari 4, 2017 katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio,  washtakiwa walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Wema anadaiwa kuwa Februani mosi, 2017 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya  aina ya bangi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles