NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MSANII wa Filamu nchini, Wema Sepetu ameamuriwa kwenda gerezani kwa siku zaidi ya saba hadi atakaporudi kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kumfutia dhamana ama la.
Mahakama imeamuru Wema aende gerezani mpaka Juni 24 mwaka huu , Mahakama itakapotoa uamuzi wa kufuta dhamana yake.
Uamuzi huo wa Mahakama umefikiwa leo Juni 17, mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde wakati mshtakiwa huyo alipofikishwa mbele yake.
Wema anakabiliwa na mashtaka ya kusambaza video ya ngono katika mitandao ya kijamii kupitia simu yake ya kiganjani.
Wakili wa Serikali Glory Mwenda amedai mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa hapo baada ya mahakama wiki iliyopita kutoa hati ya kumkamata Wema kwa kosa la kuruka dhamana.
Hakimu Kasonde alimtaka Wema kujieleza kwanini asifutiwe dhamana kwa kushindwa kufika mahakamani kwa tarehe mbili tofauti.
Akijieleza Wema alidai Mei 14 mwaka huu hakufika sababu alikuwa safarini mkoani Morogoro na Juni 11 mwaka huu aliumwa akashindwa kupandisha mahakamani.
Mshtakiwa aliomba msamaha na Wakili wa Serikali, Mwenda aliomba Mahakama impe onyo mshtakiwa ili asirudie kufanya kitendo hicho chenye usumbufu.
Hakimu Maira alisema kasikia hoja zilizowasilishwa na atapitia kiapo cha mshtakiwa kisha atatoa uamuzi Juni 24 mwaka huu na akaamuru katika kipindi cha kusubiri uamuzi mshtakiwa akae rumande.
Wema anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono katika mtandao wa kijamii.
Wema anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, ambapo alisambaza video za ngono kupitia akaunti yake ya Instagram, picha ambazo inadaiwa kuwa hazina maudhui.