NAIROBI, KENYA
MGOMBEA wa Wiper wa kiti cha ugavana wa Machakos, Wavinya Ndeti, ameshinda kesi aliyofungua dhidi ya Tume ya Uchaguzi nchini humo, IEBC, baada ya Mahakama ya Rufaa kuunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumpatia ushindi mwanamama huyo.
Wavinya alikimbilia kortini kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka wa kumpiga marufuku kuwania kiti hicho dhidi ya gavana wa sasa, Alfred Mutua.
Mahakama ya Rufaa ilitoa umuzi huo jana, kuunga mkono hukumu ya Mahakama Kuu ya kumruhusu kugombea kiti hicho.
IEBC ilitaka Wavinya kuzuiwa kushiriki uchaguzi wa Agosti 8, ikimshutumu kwa kuwa mwanachama wa vyama viwili vya kisiasa.
Tume hiyo ilisema kuwa, Wavinya hakujiuzulu kutoka kwa Chama Cha Uzalendo kama inavyohitajika kabla ya kuhamia Wiper.
Awali kabla ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Juni 21, mwaka huu na Mahakama Kuu kupitia Jaji George Odunga, kwamba Wavinya anazo sifa za kuwania kiti hicho, kwa sababu ni mwanachama kamili wa Wiper.
Wavinya sasa anatarajiwa kukabiliana na Gavana wa Machakos, Alfred Mutua, katika vita kubwa ya kiti hicho. Wavinya alikuwa amepania kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kama gavana 2017.