NAIROBI, Kenya
MAHAKAMA Kuu ya Kenya imeamuru mgombea urais wa chama cha Thirdway Alliance, Dk. Ekuru Aukot aliyekuwa ameshiriki uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu, ashirikishwe kwenye uchaguzi wa marudio uliopangiwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu.
Awali Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliwatangaza wagombea wawili pekee, Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) kushiriki uchaguzi huo, lakini juzi Odinga alitangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Maofisa wakuu wa IEBC walikutana jana kutafakari kuhusu hatua za kuchukua baada ya Odinga kujitoa.
Kujumuishwa kwa mgombea huyo kuna maana kwamba IEBC haiwezi kumtangaza Kenyatta kuwa mshindi wa moja kwa moja hata baada Odinga kujiondoa.
Dk. Aukot ni mtaalamu wa masuala ya katiba ambaye alikuwa mkurugenzi na ofisa mkuu mtendaji wa kamati ya wataalamu iliyohusika kuandika rasimu ya Katiba ya Kenya iliyoanza kutekelezwa mwaka 2010.
Wakati huohuo, Bunge jana lilipitisha miswada miwili ya kubadili sheria za uchaguzi, hatua ambayo imekuwa ikipingwa vikali na Nasa.
Marekebisho hayo saba katika sheria za uchaguzi yalipitishwa na wabunge wa chama cha Jubilee, baada ya kuwasilishwa bungeni na kamati iliyoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini, William Cheptumo.
Habari nyingine zilisema polisi wa Kenya jana waliwafyatulia mabomu ya kutoa machozi wafuasi wa Nasa waliokuwa wakiandamana katika maeneo mbalmbali ya nchi hiyo, ikiwa ni siku moja baada ya Odinga kujitoa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa urais wa marudio.
Rais Kenyatta anasisitiza kuwa uchaguzi huo wa marudio, Oktoba 26 ni lazima ufanyike kama ulivyopingwa lakini Odinga anasema hatua yake hiyo inamaanisha Tume ya Uchaguzi haina kuanza upya mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho yanayotakiwa na chama chake.
Nasa kimesema kitakuwa kinafanya maandamano lkila siku kuanzia wiki ijayo ili marekebisho hayo yaweza kutekelezwa.